Kama wewe ni mpenzi wa matangazo ya redioni,hususani ya idhaa za kigeni,basi jina la Mohamed Abdulrahman(pichani)kamwe haliwezi kuwa geni kwako. Huyu ni mmojawapo kati ya watangazaji mahiri na wakongwe ambao nchi yetu ya Tanzania inajivunia.
Mohamed Abdulrahman hivi leo ndiye Naibu Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Deutsche Welle,inayorusha matangazo yake kutokea kule Bonn nchini Ujerumani. Radio Deutsche Welle siku hizi inarusha matangazo yake sio tu kupitia vituo mbalimbali vya redio nchini Tanzania na kote Afrika Mashariki na Kati bali pia mtandaoni.Unaweza kuyasikiliza matangazo yao kupitia mtandaoni kwa kubonyeza hapa.
Hivi karibuni tulipata fursa ya kufanya naye mahojiano haya tunayokuletea hivi leo.Kama ulikuwa unamjua Mohamed kwa sauti tu basi leo tuna furaha ya kukuletea sio tu mahojiano naye bali pia picha zake ili wakati mwingine utakapomsikia redioni uwe na picha kamili.Lakini pia ni lazima tukiri kwamba mahojiano na Mohamed ni mojawapo ya yale baadhi yenu wasomaji na wachangiaji wetu mnayoyaita “mahojiano-shule”.Unasoma mahojiano na kujifunza mambo kadha wa kadha iwe ni kuhusu jamii,historia,maisha nk.
Je unajua Mohamed ametokea wapi mpaka kufika hapo alipo?Kati ya Yanga na Simba yeye ni shabiki wa timu gani?Kwanini hatoyasahau kamwe mahojiano aliyowahi kufanya na marehemu Laurent Kabila(Rais wa zamani wa DRC)? Anasemaje kuhusu uhuru wa vyombo vya habari hivi leo?Akistaafu rasmi kazi ya utangazaji, anataka kufanya nini?Kwa hayo na mengineyo mengi,fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;
BC: Wakati mwingine huwa tungependa kuanza mahojiano bila kwanza kutaka kujua kuhusu historia ya maisha ya mtu tunayefanya naye mahojiano.Lakini kwa sababu hii ni mara yako ya kwanza hapa BC, hatuna budi kukuuliza.Unaweza,kwa kifupi tu,kutupa historia ya maisha yako?Ulizaliwa wapi,ukakulia wapi,ukasomea wapi nk?
MA: Nilizaliwa Iringa mwaka 1955 na ambapo tangu mapema miaka ya ´50 Marehemu Baba yangu alikuwa Mhandisi Public Works Department (PWD).Alihamishiwa huko kutoka Zanzibar. Miaka mitano baadae tukahamia Dar es salaam ambako tuliishi mtaa wa Ukami-Kariakoo.Nilisoma shule ya msingi kwanza Aghakhan na baadae Upanga (sasa makao makuu ya jeshi). Ama elimu ya Sekondari nilisomea Zanzibar St Joseph ( sasa Tumekuja ). Desemba 1974 , siku ambayo ilikua fainali ya kandanda kati ya Young Africans na Simba katika uwanja wa Amani kule Zanzibar, nikaelekea Uingereza na pia nilisoma nchini Urusi.
BC: Naona umeitaja Yanga kwanza, je una sababu yoyote ?
MA: Ni siku ya kumbukumbu kwangu, iliyokuwa ufunguo wa maisha yangu ya baadae na labda kwa sababu nilikua tangu utotoni mpenzi wa Yanga. (Tabasamu).
BC: Inaelekea ni mpenzi sana wa kandanda, je ni nani aliyeshinda mechi hiyo na ilikuwa ya ligi kuu au vipi?
MA: Kama sikukosea ilikuwa ni fainali ya kombe la kilabu bingwa Afrika Mashariki na Kati na Yanga ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Sunday Manara na marehemu Gibson Sembuli.
BC: Kila binaadamu huwa na hadithi au mikasa ya utotoni ambayo huwa haisahauliki.Kwa upande wako,ukikumbuka maisha ya utotoni,kabla ya kufikisha miaka kumi hivi,nini huwa kinakujia kichwani kwako mara moja?Unakumbuka mkasa gani?
MA: Kwa kweli kuna kumbukumbu nyingi. Kama nilivyoeleza awali kwa wanaoijua Dar es salaam, mtaa wa Ukami na New Street mpaka mtaa unaojulikana sasa kwa jina la Lumumba hadi Gerezani na kadhalika, yaani eneo zima la Kariakoo ndiyo iliyokuwa Dar es salaam. Kwanza kwa upande wa kisiasa, ilikua enzi ya msisimko mkubwa kwani ulikua muda mfupi tu baada ya uhuru na hivyo vigogo wote wa siasa za Tanganyika hadi Tanzania walikuwa wakionekana maeneo hayo mara kwa mara.Watu kama kina marehemu Amri Abedi, Eliufoo, Kambona, Kawawa, Songambele na wengine wengi. Sherehe muhimu zilikuwa zikifanyika sana makao makuu ya TANU mtaa wa Lumumba.Mtaa wa Ukami ulikua ni kandoni tu mwa hapo, hivyo kulikuwa na wahamasishaji kama Mzee Mwinamila, Geugeu na wengine. Kwa ufupi kisiasa ni kumbukumkbu kubwa sana kwangu.
Pili katika burudani na michezo, Kariakoo ilizaa (kama naweza kutumia neno hilo), wachezaji bora wa kandanda. Ninawakumbuka Abdulrahman Lukongo,Abdulrahman Juma, Emmanuel Albert, Arthur Mambeta, Isaac Marande, Mohamed Msomali,Boi Iddi Wickens, Kitwana Manara na hasa wachezaji chipukizi kama Kitwana Douglas, Jamil (Denis Law) Jumanne Hassan(Masimenti) Mohamed Bakari Tall na wengineo. Sasa kina Boi na Juma Bomba na Masimenti walikuwa wakitoka Shule ya Mnazi Mmoja , kituo chao cha kwanza ni Ukami ama wanatukuta tukicheza “ matatu kuondoka” au Kona” basi wanajiunga nasi kabla ya kuendelea na safari.
Wakati huo kulikuwa na timu ndogo ndogo nyingi mfano wa Saigon, Everton, Pool England, Young Kenya ,Dundee na Kahe ambazo zilizotoa wachezaji waliojiunga na timu kubwa za Yanga, Simba na Cosmopolitan na kufikia kiwango cha kuwa wachezaji wa kutegemewa kitaifa na kimataifa.
Na upande wa burundani ndiyo chimbuko la Western Jazz,Dar Jazz ama Kilwa Jazz. Upande wa magoma moto kama utakumbuka kulikua na Rifters, Sparks, Comics, Afro 70 na Safari Tripers ya marehemu Marijani. Ukipendelea taarab kulikua na Egyptian Musical Club, New Extara na Al Watan. Kwa kweli kumbukumbu ni kubwa na ndefu.
BC: Sasa ukikumbuka hayo kwa upande wa michezo , ni kitu gani ambacho utasema unakifikiri sana na labda hata kusikitika kwamba mambo hivi leo hayapo kama yalivyokuwa?
MA: Nafikiria sana kipaji cha wachezaji wa kandanda enzi zile na hasa miaka ya 70 na 80, kwa sababu baadhi walikuwa na vipaji vya kiwango cha juu kuliko baadhi ya wachezaji wa-kiafrika wanaovuma leo katika ligi za Ulaya. Mchezaji kama Maulidi Dilunga, Sunday Manara, Abdullah Kibaden au kwa upande wa Zanzibar, Salhina Maftah (kwa kuwataja wachache) hawa ni wachezaji ambao kama wangekua wanacheza leo basi nafikiri Tanzania ingeshika nafasi ya kwanza ya kuwa na wachezaji wa kulipwa nchi za nje.
Kama utakumbuka Maulidi Dilunga na Mahadhi aliyekua mlinda mlango wa African Sports ya Tanga na baadae Simba walichaguliwa kuchezea timu ya bara zima la Afrika, katika mashindano yaliyofanyika Mexico. Aidha kuna upande wa riadha pia kina Filbert Bay,Suleiman Nyambui na Juma Ikangaa.Kwa hakika kila fani ilitoa vipaji vya hali ya juu na unapoiangalia hali ya sasa inavunja moyo.
BC: Unafikiri hasa sababu ni nini ?
MA: Sababu kubwa nafikiri ni wizara kutoipa michezo umuhimu inaostahili. Miaka iliyopita wizara ya michezo ilikuwa ipo ipo tu lakini haikuwa na mipango maalum. Angalia mashindano ya Shule za sekondari yamekufa kabisa.Msisimko uliokuweko zamani wa Taifa Cup baina ya timu za mikoa ukawa haupo tena na hata mashindano ya timu za vijana yakafutwa nk.
Pamoja na hayo ni jambo la kutia moyo kwamba chini ya serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete,michezo inapewa tena kipaumbele.Lakini inahitaji mashabiki wawe na subira kidogo kwani kujenga timu kwa mfano ya kandanda kunahitaji muda na kushindwa mechi ni sehemu ya kujifunza na kujirekebisha kufanikisha azma hiyo.
BC: Mara nyingi tunapokuwa watoto huwa tunatamani kuwa watu fulani au kufanya kazi fulani pindi tukifikia umri wa kufanya hivyo.Unaweza kukumbuka kwa upande wako ulitaka kuwa nani? Je utangazaji ilikuwa ni ndoto yako tangu utotoni?
MA: Ndiyo, kwa sababu ninakumbuka wakati nilipokua mdogo, kila nikioga nilikuwa napenda kuwaiga baadhi ya watangazaji mashuhuri enzi hizo na hasa wasomaji taarifa ya habari.Kwa hiyo naweza kusema,tangu utotoni hiyo ndiyo iliokua ndoto yangu kubwa. Na zaidi nilivutiwa na Ahmed Rajab ambaye ni binamu yangu, wakati huo mbali na kuwa mtangazaji wa BBC lakini hasa alipokuwa akija likizo nyumbani na kuombwa asome taarifa ya habari TBC ( sasa Redio Tanzania )

BC: Watangazaji wengi ambao tumewahi kufanya nao mahojiano wamekuwa wakitueleza kwamba mtangazaji au watangazaji fulani na fulani ndio walikuwa wakiwavutia sana katika kazi ya utangazaji kiasi kwamba wakawa wanawaona kama role models wao na hivyo kutamani kuwa kama wao siku moja. Je na wewe una kumbukumbu za namna hiyo?Kama ndio,ni mtangazaji au watangazaji gani ambao uliwaona kama role models wako?
MA: Nimemtaja Ahmed Rajab na sio kwa sababu ni binamu yangu-hapana.Lakini wengine walio nivutia zaidi ni Marehemu Othman Magoma, Dalali Mzee , Nassor Malik na Hassan Mazoa (wote walikua BBC) na nyumbani walikua ni pamoja na Chama Omar Matata Kabla ya kwenda BBC) Mzee David Wakati na Suleiman Hega . Na ukiniuliza miongoni mwa watu niliofanya nao kazi ni nani, basi nitasema zaidi ni Denis Moyo ambaye sasa yuko Tanzania. Moyo ni mmoja kati ya watangazaji wa aina yake.
BC: Kwanini ukasema hivyo kwa sababu mara nyingi ni shida kwa binaadamu kusema fulani ni kiboko kwangu ?
MA: Sidhani kama ni shida bali nitasema ni udhaifu na pengine kutojiamini.Unajua ni lazima binaadamu yeyote ujue kwamba kuna mwingine aliyekuzidi kipaji. Hiyo ni kama wewe akili yako inavyokutuma kwamba umemzidi mtu au watu fulani.Ukiishi kwa kukumbuka hilo hutokuwa na matatizo.Kinyume chake kunajenga tabia ya wivu na kadhalika.
Ni kama katika uongozi; ni lazima kutambua kwamba hapo ni mahala pa muda. Waswahili tunasema”Mpanda ngazi hushuka”. Kabla hujafika hapo ulitanguliwa na wengine na wakaondoka na wewe pia ikifika zamu yako utaondoka kisha atakuja mwingine. Marais huja wakaondoka,serikali zinakuja zinaondoka, sasa kwanini wewe uwe tofauti? Labda la msingi ninalotaka kusisitiza hapa ni binaadamu kuepuka dharau na majivuno.Ukiishi kwa njia hiyo hautakuwa na matatizo yoyote katika jamii, labda tu mivutano midogo midogo tu, jambo ambalo ni kitu cha kawaida katika maisha ya binaadamu. Natumai nimelijibu swali lako!

BC: Kabla ya kujiunga na Radio Deustche Welle, uliwahi kufanya kazi katika sehemu zipi na kwa muda gani?
MA: Niliwahi kufanya kazi na idhaa ya matangazo ya nje ya redio Comoro, Kiswahili na kiingereza baada ya kutoka Urusi ,wakati wa utawala wa kijamaa wa Ali Soilihi,kwa muda mfupi, ambapo nilikuwa pia mkuu wa idhaa ya Kiswahili kabla ya kujiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutsche Welle,mapema miaka ya 1980.
BC: Watu wengi tumekuwa tukijiuliza kwanini nchi kama Ujerumani iwe na idhaa ya Kiswahili,mahsusi kabisa kwa ajili ya kuhudumia wazungumzaji wa Kiswahili waliopo Afrika Mashariki na Kati?Ni kwamba Wajerumani wanaipenda sana sehemu hiyo ya Afrika au nini hasa kiliwasukuma kuanzisha huduma kama hii?Unaweza pia kutupa historia ya Idhaa ya Kiswahili ya Deustche Welle kama hutojali.
MA: Kuna sababu nyingi. Nitajaribu kutoa ufafanuzi kwa muhtasari tu. Idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutsche Welle ilianzishwa mwaka 1963 na watangazaji wa kwanza walikuwa ni Marehemu Omar Juma kutoka Kenya na AbdulRahim Kahtan kutoka Tanzania. Kuundwa kwake kulikuja wakati nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zikielekea katika kujinyakulia uhuru.Wakati huo ni Tanganyika tu na Uganda zilizokua tayari huru. Tanganyika 1961 na Uganda mwaka mmoja baadae.
Tayari sehemu nyingine kulikuweko na idhaa za Kiswahili, BBC, Radio Peking na Radio Cairo nk.Usisahau ulikuwa ni wakati pia wa vita baridi. BBC wao bila shaka sababu moja wapo kubwa ni mafungamano ya Uingereza na makoloni yake ya zamani mbali na sababu za kisiasa. China nafikiri ilihitaji kuwa na idhaa hiyo ambayo ipo mpaka leo, kwa sababu ya kujaribu kutanua sera yake ya kikomunisti na mchango wake katika kusaidia ukombozi wa bara la Afrika. Ama kwa upande wa Misri, nchi hiyo ilitoa mchango mkubwa kusaidia ukombozi wa bara letu wakati wa utawala wa Gamal Abdel Nasser ikiungana na Algeria ya Ahmed Ben Bella. Mji mkuu wa Algeria-Algiers ukawa makao makuu ya umoja wa vijana wa Afrika na katibu wake mkuu kama utakumbuka alikua ni mwanahabari mashuhuri nchini Tanzania Jenerali Twaha Ulimwengu.Kwa ufupi Redio Cairo ni miongoni mwa redio zilizokua maarufu sana wakati wa vita vya kupigania uhuru.
Samahani kwa maelezo yangu marefu.Nikija kwa upande wa Ujerumani na Deutsche Welle , zaidi nafikiri ilikua ni kutafuta utambulisho,hasa kutokana na historia ya baada ya vita vya pili vya dunia na kugawanyika kwa Ujerumani mbili-Mashariki na magharibi.Wamashariki wakati huo walikuwa na Redio Berlin International wakieneza propaganda na sera yao na kulihitajika bila shaka chombo cha kupingana na hayo.
Sambamba na hayo kuna masilahi ya kiuchumi. Ujerumani ilikua pia na
mamlaka katika kile kilichokua kikiitwa Deutsche Ostafrika, Tanganyika, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo haja ya kubakia chombo kama hiki imekuwepo hadi leo kukiwa na mabadiliko ya hali duniani. Lakini ni dhahiri haja ya mataifa na watu kusogeleana zaidi nayo imeongezeka chini ya kile kinachojulikana kama “utandawazi”, kwa sababu nguzo mojawapo kubwa ya utandawazi ni mawasiliano.
BC: Baadhi ya watu wamekuwa wakitoa lawama kwa vyombo vikubwa vya habari kama hiki chenu cha Deutsche Welle kwamba nyie huwa mnasubiri vyombo vingine vidogo vidogo vya habari “viwatengenezee” watangazaji wazuri kisha nyie mje kuwachukua tu na kuanza kuwatumia tayari wakiwa na uzoefu. Wanaotoa shutuma hizo wanasema hii inasababisha nchi kama yetu ya Tanzania kila siku kupoteza watangazaji wazuri na
makini(ukiwemo wewe).Unasemaje kuhusu hilo hivi sasa ukiwa kama mmojawapo wa mabosi wa Deutsche Welle?
MA: Hapa nitasema inategemea mtu unavyoliangalia suala hilo. Kuna ukweli fulani, lakini kubwa zaidi ni suala la mtu binafsi kutaka kujiendeleza zaidi. Aidha kuna hili la masilahi ambapo siku za nyuma taaluma hii ghafla ilikua ikiwekwa nyuma kabisa bila ya masilahi ya wafanyakazi kutiliwa maanani kinyume na hali ilivyokuwa hapo kabla.
Labda niseme hili la watangazaji kuhama au kuchukuliwa kama unavyosema na vyombo vingine halihusiani na redio za nje tu, hata nyumbani kumekuweko na hali ya kuhama hama, kulingana na wapi mtu anapata masilahi bora zaidi.Hata redio hizi za nje, utakuta mtu anaondoka hapa kwenda pengine kwa sababu hizo hizo. Wakati huu wa sasa ni wakati wa ushindani .Ninakumbuka ule usemi wa “chema chajiuza na kibaya chajitembeza” au vipi ? (Tabasamu)
BC: Kila mtu,kutegemeana na ujuzi maalumu au utashi binafsi,anaweza kuwa na maana yake ya mtangazaji bora.Kwa upande wako,unatafsiri vipi dhana ya mtangazaji bora?
MA: Nitalijibu suali lako kwa kusema, kila mtu ana mtazamo wake. Wanasema kipendacho moyo dawa. Lakini mtangazaji bora kwa mawazo yangu ni yule anayefuata kanuni na taratibu za taaluma ya utangazaji na uandishi habari kwa jumla na kuwa karibu zaidi na msikilizaji. Kuwasilisha kwa msikilizaji kile unachokizungumza kwa ufasaha na hali ya kueleweka. Hapa lazima nisisitize kuwa ufasaha huo ni pamoja na lugha . Ni msikilizaji wa kuamua suala la utangazaji bora.Si katika utangazaji tu lakini hata katika uandishi pia.

BC: Kutokana na uzoefu wako ni wazi kwamba umeshawahi kukumbana na mikasa mingi kazini na pia kufanya mahojiano na watu wengi tu. Katika mikasa mbalimbali kama mwanahabari ambaye unategemewa kuipasha jamii habari za kina na ukweli,ni mkasa gani ambao hutokaa uusahau?Ilikuwaje? Na ni mahojiano gani ambayo umeshawahi kufanya na mtu na kamwe hutoyasahau?Kwanini?
MA: La mikasa naomba nisilijibu kwa sababu ni mingi. Kupewa miadi halafu mtu akakuzimia simu, badala ya kukwambia kabla kwamba siwezi kuzungumza na wewe juu ya suala hilo,mtu kuwa mkali wakati wa mahojiano na mambo kama hayo.
Kuhusu mahojiano ambayo nitayakumbuka ni pamoja na Mzee Laurent Desiré Kabila nilipokutana naye katika mkutano na waandishi habari akiwa na Rais Denis Sassou Nguesso wa Congo (Brazzaville) na jioni yake kwenye ofisi yake Palais de la Nation mjini Kinshasa. Kwanza hapa pana kumbukumbu kwangu kwa sababu ni mahala ambapo Patrice Lumumba, Waziri mkuu wa kwanza wa Congo alilihutubia taifa siku ya uhuru. Kwanini sintoisahau siku hii ? Ni kwa sababu niligundua Mzee kabila alikua tofauti na vile alivyokua akiripotiwa na baadhi ya magazeti ya kigeni. Na pia nilipata kujionea na kujifunza mengi kuhusiana na hali halisi ya Congo wakati ule. Ilikuwa ni wiki chache baada ya kurudi Cologne ambapo Mzee Kabila aliuawa na mmoja wa walinzi wake tarehe 16 Januari, 2001.
Mazungumzo mengine ya kusisimua yalikuwa na rais wa sasa wa Burundi Pierre Nkurunziaza mjini Bujumbura baada ya kutoka msituni, wakati akiwa Waziri wa nchi anayehusika na utawala bora katika serikali ya mpito ya Domicien Ndayizeye.
Mahojiano mengine ambayo yalikuwa ya kusisimua kwangu ni pamoja na Dr. Salim Ahmed Salim wakati alipokua Katibu mkuu wa umoja wa Afrika(OAU) juu ya migororo ya bara la Afrika.
BC: Na ni kiongozi gani ambaye kwa sasa ungependa kukutana naye kwa mahojiano ?
MA: Wako wawili watatu lakini miongoni mwao ni Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete?
BC: Kwanini ?
MA: Kwa mawazo yangu ni kiongozi mwenye mvuto na kizazi kipya cha uongozi barani Afrika.
BC: Unafikiri kipi ambacho Tanzania inaweza kujivunia?
MA: La kwanza utulivu na hapa lugha ya Kiswahili imesaidia sana katika hilo, ingawa siku hizi kumeanza kuzuka mtindo wa kikabila kwa mtazamo wangu binafsi.
BC: Unaweza kufafanua ?
MA: Ndiyo kwa sababu zamani ukisema nimetoka Tanzania ilikua inatosha lakini sasa kuna swali la ziada, Tanzania wapi ? Hapa kuna ncha mbili kweli mtu anaweza kukuuliza kutaka kujua ni sehemu gani ya Tanzania , lakini baadhi ya wakati kuna hisia za kutaka kujua wewe ni mtu wa sehemu gani katika misingi ya kikabila au hata dini na hii ni hatari.
Jambo la pili la kujivunia mbali ya lugha, mshikamano na utulivu ni mchango wa Tanzania katika ukombozi bara la Afrika. Dar es salaam yalikua makao makuu ya vyama mbali mbali vya ukombozi, kuanzia ZANU (Zimbabwe), ANC na PAC (Afrika kusini) ,SWAPO (Namibia), MOLINACO (Comoro) SPUP (Ushelisheli au Seychelles) bila kuisahau FRELIMO ya Msumbiji. Ni mchango mkubwa katika utu na ukombozi wa mwaafrika na hilo ni la kujivunia sana .
BC: Nini unakipenda zaidi na kipi hukipendi katika kazi yako ya utangazaji au uana habari kwa ujumla?
MA: Dooh ! ni swali gumu hilo. Kwa ufupi chochote nitakachoweza kukitekeleza kufanikisha jukumu langu kwa ufanisi.
BC: Suala la uhuru wa vyombo vya habari ulimwenguni,hususani kwenye nchi za kiafrika,bado linaendelea kugubikwa na kiwingu fulani.Wengine wanasema uhuru wa vyombo vya habari upo, wengine wanasema haupo,wengine wanasema upo na hata umezidi au kuvuka mipaka. Nini maoni yako kuhusiana na hili?
MA: Inategemea unavyoliangalia na inategemea nchi na nchi. Vile vile ni jambo linaloambatanishwa na masilahi.Lakini kanuni za uhuru wa vyombo vya habari zinafahamika kote duniani na hazitofautiani hata kidogo. Bila shaka kila kitu kina mipaka yake, hawezi tu mtu kubisha hodi nyumbani kwako, kwa mfano, na kufululiza moja kwa moja chumba chako cha kulala. Ukweli na habari za kuaminika ndiyo msingi mmoja wapo wa uhuru huo.
Na kwa upande wa pili kukosolewa chini ya msingi huo kusiangaliwe kuwa ni dosari bali changamoto kuweza kujikosoa na kujirekebisha na process hiyo kwa jumla ni msukumo katika kupiga hatua moja mbele.
BC: Kwa watu wengi,kutokana na hadithi na simulizi mbalimbali,Ujerumani ni nchi iliyojaa ubaguzi wa rangi kushinda mataifa mengine ya Ulaya na hata Marekani ya kaskazini.Upi ukweli?Je wewe binafsi umeshawahi kukutana na mikingamo hii ya ubaguzi wa rangi?
MA: Visa vya ubaguzi viko kila mahala duniani hata nyumbani Afrika kuna visa vinavyoangaliwa kama vya kibaguzi. Mvutano na hata mapigano baina ya jamii mbili tafauti au makabila tafauti pia ni sehemu ya ubaguzi. Kwa Ujerumani kuna matukio ya aina hiyo dhidi ya wageni, lakini mara nyingi nafikiri yanatokana na hasira zisizo na msingi na pia ujinga. Kwa sababu unaposema unampiga daktari wa kigeni kwa kisingizio wageni wanachukua nafasi za kazi ni ujinga, wakati wewe unayelalamika hukumaliza masomo hata ya sekondari na huyu akiondoka huwezi kujaza pengo aliloliacha.
Kwa upande wangu siku wahi kukutana na visa vya aina hiyo, ingawa unakutana na watu wenye masuali ya kijinga baadhi ya wakati. Lakini muhimu zaidi kama ngao ,kupambana na ubaguzi mahala popote ni kuwa karibu na jamii ya pale (integration) na kujifunza lugha.
BC: Una mipango gani baada ya kustaafu ?
MA: Ni mapema mno kusema nitafanya nini kwa sababu bado njia ni ndefu,lakini panapo majaaliwa Mwenyezi Mungu akipenda nia yangu ni kurudi nyumbani Kijitonyama na pengine kuandika kitu juu ya maisha yangu ?
BC: Historia yako inaanzia mtaa wa Ukami na sasa naona unataja Kijitonyama,Kwanini, Kijitonyama ?
MA: Kwanza kwa sasa hapo ndipo alipo Mama yangu na niseme familia, labda ni vizuri nipaite makao yangu makuu.Pili, ningependa kubakia mtu wa kawaida kwa maana ya kuishi na watu. Hili nimejifunza kutokana na maisha na wasia wa Wazee wangu wawili waliokua karibu sana, mjomba wangu Mzee Aboud Mahmoud Maalim na kaka wa baba yangu Mzee Ali Mohamed Rajab (makopo).Mzee Maalim mbali na kuwahi kushika nyadhifa kadhaa za juu katika serikali ya Muungano na Zanzibar wakati wote alikuwa mtu wa watu na alichukulia mengine kuwa ni mambo ya kupita tu. Kadhalika Mzee Rajab alikua pia mtu wa watu na wa msaada. Wote bahati mbaya sasa ni marehemu lakini ni wao pamoja na Mama yangu Mzazi ambao ni kioo cha maisha yangu. Kwa muhtasari kulijibu swali lako. Ni muhimu kwa binaadamu kukumbuka alikotoka.
BC: Naomba kabla ya kumaliza mahojiano haya kukuuliza swali binafsi kidogo kama hutojali.Umeoa?Una watoto?Wangapi?
MA: Naam nimeowa , mke wangu anaitwa Maryam Abubakar alikua Air Hostess Shirika la ndege la Tanzania ATC zamani na nina watoto watatu, Abdullatif, Kamal na Nadya.
BC: Nashukuru.Unalo lolote ambalo ungependa kuongezea au kwa faida tu ya wapenzi na wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Deutsche Welle?
MA: Sina isipokua tu kukushukuru wewe na kukutakia pamoja na wasikilizaji wa Deutsche Welle kila la kheri, afya njema na usikilizaji mzuri.
BC: Ahsante kwa muda wako.Tunakutakia kila la kheri katika kazi zako.
MA: Ahsante sana na kwako pia kila la kheri!
Feedback / Comments
11 Responses to “TULIPOKETI NA MOHAMED ABDULRAHMAN”
Leave a Reply


Kwa miaka chungu mbovu nimekuwa nikimsikia huyu bwana radioni.Nilikuwa sijawahi kumuona alivyofanana.Inatia hamasa na raha sana kumuona hapa.By the way..kazi nzuri sana mnafanya hapo Deutsche Welle.Nawasikiliza sana mtandaoni.Good job BC.
Heko bwana Abdulrahmani. Wewe na redio yenu nimewavulia kofia kwa upande wa lugha fasaha. Mnajuwa kuchaguwa watangazaji. Yaani wengi wenu hapo Radio Deutsche Welle mnaongea kiswahili safi, siyo kama hizi redio nyingine ni kama vile wanaokotaokota watangazaji ambapo mtu utakuta anasema IMENIADHIRI badala ya IMENIATHIRI, GAFLA badala ya GHAFLA, GALI badala GHALI, WAMEDHIBITISHA badala ya WAMETHIBITISHA, TAFAZALI badala ya TAFADHALI, wakati mwingine wanasema DHAMINI mahali inapotakiwa waseme THAMINI. Hawajui kuwa wanapotosha kabisa hata maana ya wakisemacho wakati mwingine.
Nyinyi hamna upuuzi huo, nakupongeza wewe na watangazaji wenzio wa redio yenu. Nyinyi mnaongoza na wengine wanafuata.
Mimi.
Yaani leo ndo nimeweka mbili na mbili pamoja. Namsikiliza sana huyu muheshimiwa mtandaoni lakini ndo hivyo nilikuwa sijapata kumtia machoni. Tunaomba na watangazaji wengine pia kama akina Samia Othman…..nk.
Kazi nzuri………..
Deutsche Welle ya akina Mohammed Abdulrahman ipo katika nafasi nzuri ya kuwazidi kete BBC ambao kwa muda mrefu wamekuwa na idadi kubwa ya wasikilizaji – milioni 20 na ushee.
Sababu mojawapo ni lugha mbovu inayotumiwa na watangazaji wake wenye asili ya Kenya au wakenya.Tangu wahamishie matangazo yao ya alfajiri Nairobi kumekuwa na kila aina ya “ubakaji wa lugha ya kiswahili”.
Lafudhi ya ovyo, misamiati duni na mtiririko wa maneno ni wa kubabaisha.Tangu Tido Mhando aondoke mambo yamekuwa yakienda kombo BBC – matangazo ya asubuhi, Dira ya Dunia bado inajitahidi.
Mohammed kaza uzi, hao BBC waendelee na kiswahili chao kibovu – mojawapo ya sifa zao ilikuwa lugha nzuri, sasa kama haipo nani atawasikiliza watu wanaosema jambo moja kumbe wana maana nyingine [kudhibiti na kuthibitisha].
Tatizo la Deusche Welle ni mabahili [flat mean, hawawezi kushindana na bajeti nene ya BBC.Wajerumani hawana hata ofisi kwa waandishi wao East and Central Africka.Pia teknolojia ya kukusanya sauti si ya kisasa.
Huyu naye ni Bongocelebrity!!!si ni mjerumani huyu,huo utanzania kaupata wapi?????????????
Jamaa anayejiita Poul anaonyesha kuwa na chuki. Mimi sijui kama Bwana Mohamed ni mjerumani, lakini kama ni mjerumani kuna watanzania wangapi wenye kuishi nje marekani, uingereza , scandinavia,ghuba etc ambao wana uraia wa nchi hizo. Hata watoto wa wakubwa kibao uingereza na marekani wana uraia. Je hilo linawafanya wasiwe watanzania na mkipitisha uraia wa nchi mbili itakuaje. Poul angalia mbele. jamaa ni kiboko acha wivu na chuki zizizo na msingi.
Akhsanteni sana BC kwa kutuletea mahojiano na kutusaidia kupata kumuelewa ndugu Mohamed Abdulrahman, kwanza napenda kumpongeza ndugu Mohamed na watangazaji wote wa radio Deutsche Welle kwa matangazo ya wanayoturushia yenye kiswahili fasaha kwa hilo nataka kuwaambia kuwa katika radio zote za nje zinazotangaza kiswahili wao ni Alfa na Omega. Pili huyu ndugu Mohamed amenikumbusha mbali sana milango ya sabini, anaonyesha ni kweli mtoto wa Dar maana alivyonichambulia timu za zamani Dar,Bendi za muziki na Taarab ukiachilia wanasiasa namvulia kofia. Tatu tukirejea kuhusu mdau anayejiita Poul nadhani huyu bwana ana chuki zake binafsi na roho ya kwanini (kikorosho). kama anasema kwamba ndugu Mohamed si mbongo ni mjerumani, basi hiyo itakuwa ndugu Mohamed ni kwa ajili ya kutafuta maslahi na pia ndugu Poul ahisi fahari kwa kusikia ndugu Mohamed kuwa ikistaafu anatarajia kurudi nyumbani na nyumbani kwenyewe kijitonyama uswahilini. sio Berlin au Hamburg. nilikuwa namuomba ndugu Poul awe na wivu wa kimaendeleo sio wivu wa chuki na kwa nini nyingi. mwisho nilikuwa na muomba ndugu Mohamed yeye na wenzie wazidi kuturushia matangazo kama kazi wasikatishwe tamaa na kelele za mlango ambazo hazitomfanya mwenye nyumba kukosa kulala.
ni mimi Zee la kitaulo
mimi nimefurahishwa na historia fupi ya mtangazaji mohamedi abdulrahman,miminiseme tu kwa uchache kuwa nimwakilishi mzuri wa nchi yetu.ingawa kuna walio mponda nawaombea msamaha kwani hajui walisemalo.pia abbakary liongo na mpa hay kwani inaonyesha wazi tanzania tulivyo na mabalozi wenye kujituma.sio hao tu wapo chipkizi kama Scolastika Mazula.nawaombeni fanyeni kazi kwabidii ili wenye wivu waji nyonge.wenu msikilizaji maarufu wa RW KAZI NJEMAMA
Bwana PAUL wacha chuki binasfi haifai, Mohamed Abdulrahman ni mtz tena wa nguvu kabisa, mimi ni jirani yake hapa sinza na ukipata muda uje tukupeleke hadi kwao.
big up bro M.A. tunawashukuru sana kikosi kizima cha DW kwa kutuwakilisha huko ujerumani na dunia nzima.
take care bro
HUWEZI KUWA MTIIFU AU MUADILIFU KTK TAIFA HILI,,,UNAWEZA KUWA NA VETI VYA KILA AINA LAKINI USIWE MUADILIFU,,,, JE UFANYE NINI UWE MUADILIFU NA MTIIFU KTK JAMII ????
LAZIMA UPITE ZANZIBAR ,,, JE YUPO ANAYE PINGA ?
Una historia ya kuvutia Bw Mohammed