MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

Raisi Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Prof.Benno T.Ndulu (pichani) kuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BOT). Uamuzi huo umefuatana pia na maamuzi mengine mazito kama ambavyo yameanishwa katika taarifa rasmi ya Ikulu iliyotolewa hivi leo jijini Dar-es-salaam. Yote haya yanafuatia utata na sakata zima lililokuwa limeigubika Benki Kuu ya Tanzania.

Wakati huo huo Raisi Kikwete amemteua Dr. Enos S.Bukuku kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu. Taarifa rasmi ya Ikulu unaweza kuisoma hapa.

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI WA HESABU KATIKA AKAUNTI YA MALIPO YA MADENI YA NJE (EXTERNAL PAYMENT ARREARS ACCOUNT – EPA) ILIYOKO BENKI KUU YA TANZANIA.

Nafurahi kuwaarifu kuwa, kazi ya Ukaguzi wa Hesabu za mwaka wa fedha 2005/06 za Akaunti ya Madeni ya Malipo ya Nje yaani External Payment Arrears (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania imekamilika. Kazi hiyo ilifanywa na Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Ilianza Septemba, 2007 na kukamilika Desemba, 2007. Juzi tarehe 07 Januari, 2008 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alikabidhiwa Taarifa hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Rais ameisoma, ameifanyia kazi na kuitolea maamuzi.

Historia ya EPA

Katika miaka ya 1970 mpaka 1990 nchi yetu ilikuwa inakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa fedha za kigeni. Benki Kuu ya Tanzania ilipewa jukumu la kusimamia matumizi ya fedha za kigeni kwa niaba ya Serikali. Benki Kuu ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kupanga na kuamua nani agawiwe fedha za kigeni na kiasi gani!

Kwa ajili ya kuwahudumia wafanyabiashara, mashirika na makampuni yanayoagiza bidhaa na huduma kutoka nje, Akaunti maalum ilifunguliwa katika Benki ya Taifa ya Biashara kwa wakati huo. Akaunti hiyo ilijulikana kwa jina la External Payment Arrears (EPA) au Akaunti ya malipo ya Madeni ya Nje, kwa tafsiri ya Kiswahili.

Waagizaji wa bidhaa au huduma kutoka nje waliwajibika kulipa kwenye Akaunti hiyo, fedha ya Tanzania yenye thamani inayolingana na fedha za kigeni zinazotakiwa kulipia bidhaa au huduma hiyo huko nje. Baada ya waagizaji wa ndani kufanya hivyo, kutegemeana na upatikanaji wa fedha za kigeni, wauzaji au watoaji huduma wa nje walilipwa. Benki Kuu iliamua nani alipwe na Benki ya Biashara ilifanya malipo.

Juni, 1985 iliamuliwa kuwa shughuli za akaunti hiyo zihamishiwe Benki Kuu kutoka Benki ya Taifa ya Biashara na zimeendelea kuwepo hapo mpaka sasa. Katika Benki Kuu kikaundwa kitengo maalum cha kusimamia na kuendesha shughuli za akaunti hiyo kilichojulikana kama Debt Management Unit chini ya Kurugenzi ya Sera (Directorate of Economic Policy).

Kwa sababu ya tatizo la upungufu wa fedha za kigeni kuendelea, malimbikizo ya madeni hayo yalizidi kukua mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 1999 deni hilo lilifikia dola za Kimarekani 623 milioni. Kati ya fedha hizo, dola 325 milioni ndilo deni la msingi na dola 298 milioni ni riba yake. Baadae likaongezeka kufikia dola 677 milioni.

Juhudi za Kulipa Madeni

Juhudi za kulipa malimbikizo ya madeni hayo ziliendelea kadri fedha za kigeni zilipopatikana. Kwa nia ya kutaka kutafutia ufumbuzi wa haraka tatizo hilo na kupunguza mzigo wa madeni, Serikali ilianza kutafuta njia nyingine mbalimbali. Mwaka 1994, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ilianzisha Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme). Yaani waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya madeni wanayodai. Wapo wadai kadhaa walikubali na madeni yao yakauzwa chini ya mpango huo. Taarifa za mwaka 2004 zinaonyesha kuwa madeni ya thamani ya dola 228 milioni yalilipwa chini ya mpango huu.
Pili, Serikali ilifanya juhudi ya kupata msamaha wa madeni hayo kutoka nchi wanachama wa Paris Club. Serikali iliomba kuwa pamoja na kutusamehe madeni ya kiserikali toka nchi zao wasaidie tusamehe na madeni ya makampuni yao kwetu. Yapo pia madeni ambayo yamelipwa na makampuni ya Bima baada ya makampuni yaliyouza bidhaa na huduma Tanzania kushindwa kulipwa. Madeni ya dola 216 milioni yalihusika chini ya michakato hii. Hivyo basi, deni la dola 444 milioni lilipungua katika ile jumla ya dola 677 milioni. Kwa hiyo mwaka 2004 deni katika Akaunti ya Malipo ya Nje lilikuwa dola 233 milioni. Yalikuwepo mawazo ya baadhi ya watu kuwa pengine deni hilo lisilipwe au tulikatae. Walikuwepo waliokubali madeni yao yafutwe na wengine waliagiza fedha zao zipewe NGO. Lakini, baadhi ya wadai waliendelea kudai na wengine hata kushitaki mahakamani. Hivyo BoT ililazimika kuendelea kulipa kadri wadai walipojitokeza.

Ulipaji kwa Idhini

Katika utaratibu wa malipo ya madeni ya EPA kanuni zinaruhusu mdai kuamua deni lake kulipwa kwa mtu au kampuni nyingine. Kanuni zinamtaka mdai kutoa hati iliyothibitika kisheria ya yeye kuidhinisha malipo hayo yafanywe (Notarised Deeds of Assignments) hivyo. Pia yapo masharti ya kutimizwa na kampuni au mtu aliyeidhinishwa kulipwa hilo deni. Utaratibu umetumika kufanya malipo kadhaa ya madeni katika Akaunti ya EPA.

Matatizo ya Mwaka 2005/6

Katika ukaguzi wa Hesabu za BoT za mwaka wa fedha 2005/6, Agosti, 2005 kuligundulika matatizo katika ulipaji wa madeni kwa utaratibu wa idhini ya kulipwa wakala wa mdai katika akaunti ya EPA. Kukajitokeza kutokuelewana kati ya Benki Kuu na Mkaguzi Deloitte and Touche’ aliyegundua tatizo hilo. Baadaye mkaguzi huyo alisitishwa kuendelea na kazi. Serikali ikaingilia kati na tarehe o4 Desemba, 2006 ilimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikisha kuwa ukaguzi wa akaunti hiyo unafanyika kwa kina. Aidha, ilimuagiza atafute kampuni ya kimataifa ya ukaguzi ifanye kazi hiyo kwa niaba yake. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali, ndiye kwa mujibu wa Sheria ya BoT mkaguzi wa Hesabu za Benki Kuu. Hata hivyo kwa mazingira hayo maalum Serikali ilimtaka CAG atafute mkaguzi mwingine wa nje.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya hivyo na matokeo ya mchakato wa kutafuta kampuni hiyo uliochukua miezi mitano (Januari hadi Mei, 2007) ndipo ikapatikana kampuni ya Ernst and Young.
UKAGUZI

Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young wakaanza kazi hiyo Septemba, 2007 na kuikamilisha Desemba, 2007. Wakaguzi hao wamefanya kazi nzuri iliyothibitisha kiwango cha juu cha weledi (Professionalism) cha wakaguzi hao. Tunawapongeza, tunawashukuru. Tunatambua kuwa walipata matatizo mengi hasa ya kupata taarifa zilizo sahihi kwa sababu ya matatizo ya utunzaji wa kumbukumbu. Madeni haya ni ya miaka 27 na zaidi iliyopita. Kumbukumbu zimehamishwa kutoka NBC kwenda BoT. Hata huko NBC shughuli zilikuwa zinafanywa katika matawi mbalimbali nchini tena miaka hiyo hapakuwa na kompyuta hivyo kumbukumbu zote ziliwekwa kwenye majalada. Pamoja na matatizo hayo ukaguzi wa hesabu za mwaka 2005/6 ulikamilika kwa kiwango cha kuridhisha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ukaguzi katika mwaka wa fedha wa 2005/2006 uliochunguzwa, katika mwaka 2005 yalifanywa malipo ya jumla ya Shilingi 133,015,186,220.74 kwa Makampuni 22 ya hapa nchini. Makampuni hayo ni: Bencon International Ltd. of Tanzania, VB & Associates Company Ltd. of Tanzania, Bina Resorts Ltd. of Tanzania, Venus Hotel Ltd. of Tanzania, Njake Hotel & Tours Ltd., Maltan Mining Company Ltd. of Tanzania, Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment Ltd., B. V. Holdings Ltd., Ndovu Soaps Ltd., Navy Cut Tobacco (T) Ltd. of Tanzania, Changanyikeni Residential Complex Ltd., Kagoda Agriculture Ltd., G&T International Ltd., Excellent Services Ltd., Mibale Farm, Liquidity Service Ltd., Clayton Marketing Ltd., M/S Rashtas (T) Ltd., Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na KARNEL Ltd.

Aidha, ukaguzi umebaini kwamba kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 90,359,078,804.00 zililipwa kwa makampuni kumi na tatu (13) ambayo yalitumia kumbukumbu, nyaraka na hati zilizo batili na za kugushi. Hivyo, Makampuni hayo hayakustahili kulipwa chochote. Makampuni hayo ni: Bencon International Ltd. of Tanzania, VB & Associates Company Ltd. of Tanzania, Bina Resorts Ltd. of Tanzania, Venus Hotel Ltd. of Tanzania, Njake Hotel & Tours Ltd., Maltan Mining Company Ltd. of Tanzania, Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment Ltd., B. V. Holdings Ltd., Ndovu Soaps Ltd., Navy Cut Tobacco (T) Ltd. of Tanzania, Changanyikeni Residential Complex Ltd., Kagoda Agriculture Ltd.

Aidha, ukaguzi umeendelea kubaini kuwa Makampuni tisa (9) ambayo yalilipwa jumla ya Shilingi 42,656,107,417.00 hayakuwa na nyaraka za kuonyesha stahili ya malipo na hivyo kuwafanya wakaguzi washindwe kuhakiki uhalali wa malipo hayo. Makampuni hayo ni: G&T International Ltd., Excellent Services Ltd., Mibale Farm, Liquidity Service Ltd., Clayton Marketing Ltd., M/S Rashtas (T) Ltd., Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na KERNEL Ltd.

Wakati huo huo Makampuni mawili, yaani, Rashtas (T) Ltd na G&T International Ltd., kumbukumbu zake za usajili katika daftari la Msajili wa Makampuni nchini hazikuweza kupatikana.

Uamuzi wa Rais

Baada ya kuipitia Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na ya Mkaguzi wa Nje, yaani, Kampuni ya Ernst and Young, Mhe. Rais amesikitishwa na kukasirishwa na taarifa ya kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti kama vile Benki Kuu. Kwa hiyo, ameamua kuwa hatua za kisheria na kiutawala zichukuliwe dhidi ya makampuni na watu waliohusika na vitendo hivyo viovu.

Kwa ajili hiyo Rais ameamua yafuatayo:-

1. Ametengua uteuzi wa Dkt. Daudi A. Balali kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

2. Ameagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ikutane mara moja kujadili taarifa ya ukaguzi na kuchukua hatua zipasazo za kinidhamu dhidi ya Maofisa wote wa benki, walio chini ya mamlaka yake waliohusika na kusababisha hasara hii kwa taifa.

3. Shughuli za ulipaji wa madeni katika Akaunti ya EPA zisimamishwe mara moja mpaka hapo taratibu za uhakiki na utaratibu mpya utakapotengenezwa.


4. Rais amewaagiza; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kuchunguza na kuchukua hatua zipasazo za kisheria kwa makampuni na watu waliohusika na uhalifu huu. Rais amewataka watumie ipasavyo mamlaka na madaraka waliyo nayo kwa mujibu wa sheria. Aidha, amewataka wakamilishe kazi hiyo katika kipindi cha miezi sita. Amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali awe kiongozi wa kazi hii. Amewataka wahakikishe kuwa fedha zilizolipwa isivyo halali zinarudishwa.

5. Rais pia amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kushirikiana na kuwasaidia watendaji wakuu hao wa vyombo vya dola katika kufanikisha jukumu lao hilo. “Watu wengine wenye taarifa za ziada pia wazitoe kwa Timu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake”.

6. Kutokana na hatua ya kutengua uteuzi wa Bwana BALALI, Mhe. Rais amemteua Prof. BENNO T. NDULU (Naibu Gavana) kuwa Gavana Mpya wa Benki Kuu. Halikadhalika, amemteua Dkt. ENOS S. BUKUKU (Katibu Mkuu – Miundombinu) kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu (Fedha na Uchumi). Pia amemteua Ndugu Omari Chambo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu. Uteuzi huu unaanza mara moja.

(Phillemon L. Luhanjo)

KATIBU MKUU KIONGOZI

IKULU,
DAR ES SALAAM
09 Januari 2008

Share and Enjoy:
  • Digg
  • Sphinn
  • del.icio.us
  • Facebook
  • Mixx
  • Google Bookmarks
  • email
  • LinkedIn
  • Live
  • Spurl
  • Technorati
  • Yahoo! Buzz
  • YahooMyWeb

Feedback / Comments

26 Responses to “PROF.BENNO NDULU,GAVANA MPYA BENKI KUU.”

  1. Comment by Chris on January 9th, 2008 12:01 pm

    Simba ameunguruma. Kama ni maamuzi kwa manufaa ya Taifa la Tanzania leo Kikwete amelitoa. Na kuwaagiza TAKUKURU, AG, CAG na IGP kufanya hiyo kazi nimemsifu maana ni amewapa meno ambayo walikua nayo ila hawakutaka kuyatumia,sijui kama nao ni mafisadi. Kwanza ni aibu kwao maana ilibidi wafanye kazi hiyo kabla Raisi hajawaambia.

    Ila nina utata na Uteuzi wa Prof. Ndulu,huyu jamaa kama alikua anakula na Dr Balali (kama ikidhihirika) itakuwaje?. Nafikiri angeteuliwa Gavana mpya from out of BoT system kama Dr Bukuku. Personally nilibahatika kufanya kazi na Dr. Bukuku time akiwa Katibu Mkuu, Mipango na Ubinafsishaji. (nilikua nafanya research yangu pale). Ni mchapa kazi kazini alikua anatoka saa 5 au nne usiku.nakumbuka kuna siku kulikua na zengwe ofisini aliwaita wakurugenzi saa 4 usiku waende ofisini for emergence meeting. Jamaa ni mchapa kazi nampongeza Mh. Raisi kwa kuona jinsi alivyo hazina. He’ll take us a place Tanzanians need.

    Naomba waliomriwa kufanya kazi na Raisi walifanikishe hilo swala,japo miezi sita ni mingi sana.Tanzania kunakuwaga na zima moto then kila kitu kinasahauliwa katika kati. Wawajibishwe iwe fundisho kwa wote mafisadi. Lakini kikubwa nafikiri hiyo hela kama alivyoagiz Raisi irudi but irudi na RIBA,maana kama ni faida imeshawatengenezea sana.

    MUngu Ibariki Tanzania, na Raisi wetu Kikwete ambae binafsi kwa maamuzi haya Naanza pata imani nae.

    Chris, The Netherlands.

  2. Comment by Mama wa Kichagga on January 9th, 2008 2:27 pm

    This is a wonderful team!

    Congratulations kwa Gavana mpya na naibu wake!

    Sina wasiwasi kabisa na utendaji wa Bukuku maana alinifundisha uchumi UDSM na ni mkali ktk masuala ya uchumi kwani pia alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Mipango na Uchumi!

    Vitoto vya ubadhirifu BOT mkae mkao wa kuondoka maana Dr. Bukuku hali wala hapokei rushwa! Hata kama wewe ni mtoto wa mkubwa haangalii yeye anaangalia utendaji, kama uko goi goi off you go! Ukikalia fail unalo ndugu analijia mwenyewe hukohuko uliko! Safi sana!

    Nampongeza Rais wetu kwa uteuzi huu makini na maamuzi haya mazito hasa katika jamii yetu ya Kitanzania! Sasa nchi inaanza mwendo wa kasi!

    Badili kila mahali panapoonekana kukuzorotea juhudi zako mheshimiwa!

    Nampenda Rais wangu ni muwajibikaji na Mzalendo! Mungu aendelee kutubariki tuuondoe huu umaskini kabisa uliokidhiri!

  3. Comment by Daktari on January 9th, 2008 4:14 pm

    Hongera Prof Ndullu,
    Ninapenda kumpongeza Prof Ndullu kwa kuwa rasmi gavana wa BOT,jamani huyu ni mtu makini asiye penda kuyumbishwa na mwenye msimamo usio pinda hakika ni kichwa.Jamaa unayefikiri huyu alikuwa akishirikiana na Balali umekosea kwani Ndullu kaja BOT muda mfupi tu kumbuka tulikuwa hatuna post za manaibu gavana na zilipoanzishwa yeye ndo aliteuliwa na JK kuwa mmoja wapo ila puppet wa Ballali ni juma Reli ambaye ndiye aliyeachiwa post but JK kampa rungu Ndullu na bukuku.
    Huu ni mwanzo wa maovu yaliyopo Tz na hakika mengi makubwa yaja na yatawahsangaza wengi but maombi ya wenye haki hujibiwa daima.
    Thanks

  4. Comment by Edwin Ndaki on January 9th, 2008 4:58 pm

    Binafsi sioni cha kupongeza hapa.Narudia tena BINAFSI.

    Eti..kamfukuza!! kamfukuza wakati balali alisoma alama za nyakati akajua ili zengwe zito akaamua kutembea zake mbele.
    Aliandika baraua ya kujiuzulu,nafikiri wakaona wazime issue wakadai hajajiuzuri ili wamtimue.

    Ninatamwona JK kanya jambo la maana hapo nitakapo waona wote waliohusika kwenye ilo sakata wanafikishwa mbele ya sheria.

    Jamaa katumbua mabilioni.Eti adhabu yake anafukuzwa kazi..kituko.

    Kibaka kaiba mia tano,wanapiga hadi wanaua.Hukuma za kitanzania si zielewe.

    Tatizo wanaogopa kumpeleka balali kwenye vyombo vya sheria kwa maana atawataja aliokuwa anakula nao,ambao unaweza kuta ndio hao hao wanene wa nchi.

    Hata huyu aliyeteuliwa nina mashaka naye.Maana mara nyingi ayafanyao konda,dereva pia anajua.Haingii kwenye mbongo yangu kuwa huyo bwana ni clean.

    Mwanza mzuri JK,paka umetuonyesha.Asante.Nenda kamfunge kengere basi.

    wasalaaa…

  5. Comment by Wajinga wapo wengi on January 9th, 2008 6:01 pm

    They say u can lead horse to the water but you cant get them to drink it, he sure has shown resilience to the ungrateful Tanzanians, I will remember his reign by the history on our economic growth which has never been as high before since independence but disgustingly we let the real Wafisadi sit on it, and blame to the dignified and hardworking one? But hey time will soon tell how down hill our economy will go and then we can have a real thing to blame on , to not even be able to afford a little maharage, and fuel prices keeps on souring high with no rain in sight , then will think about how unfair to Ballali people have been. To be honest that’s not even an office to worth his time, it’s like a market – you worth more, enjoy your retirement, I dare to say a proper office, and I salute you!!!

  6. Comment by Wajinga wapo wengi on January 9th, 2008 8:14 pm

    i can just again remind all of you to visit http://www.bot-tz.org/AboutBOT/AboutDaudiBallali.htm

    before you open your mouth without no brains , hope the new governor can live up to much up Mr Ballali’s standards

  7. Comment by kimk on January 9th, 2008 9:20 pm

    Hii taarifa ni ushahidi kuwa akina Dr Salaa na Kabwe wana hoja za msingi kabisa.Isingekuwa wao nani angejua kuwa kuna kampuni hewa zilipewa pesa. Hii inadhihirisha kuwa hata mkataba wa Buzwagiambao spika aliukingia kifua usiundiwe tume una arufu hiyo hiyo.
    Kwa hili wapinzani wamefanya uzalendo wa kweli.Sasa wale waliotaka kwenda kumshataki Dr Salaa tunawasubiri waende.

  8. Comment by Majita on January 9th, 2008 10:36 pm

    KWA WADANGANYIKA WOTE:-
    Ifuatayo ni historia ya Dr.Balali.
    1:First Degree 1961-Harvard-(Boston) MA USA.
    2:Masters Degree 1964-Washington-USA.
    3:Phd 1967-Washington-USA
    4:Kazi IFM kwa miaka 23-USA.
    5:1997 aliazimwa na serikali ya Tanzania kuwa mshauri wa uchumi akitokea USA
    6:1998 Gavana wa BoT na familia yake inaisi Washington USA
    7:2007 kuugua na ETI kulazwa Boston MA-USA.
    ©Majita
    Hahahahahahahahaha.LoL.Sina mbavu.Mwenzenu ndo kafika home kwa familia yake.Kamwe na narudia KAMWE Balali hamumuoni TZ tena.Keshawapiga nyie changa la macho.

    Hivi mnafahamu huyu mdudu “Mensons au Mesonic au freeMesonic???” Huyo ndo mlezi wake Dr.Balali.

  9. Comment by Queen on January 10th, 2008 1:51 am

    Hongera kwa Rais wetu Kikwete mi nimefurahi saaaaana.Ile taarifa ya Luhanjo ingenoga zaidi ungeisomwa mwenyewe manake wangekuona ulivyokasirishwa lakini hata hivyo ilikuwa na utamu wake ilivyosomwa na Katibu Mkuu Kiongozi.
    Nilichokiona mimi ni kwamba sasa watanzania tunaamka,hakuna mambo ya kuangalia sura.Wapinzani Hongereni sana tunaiona kazi yenu,lazima Utawala bora uwepo Tanzania.Nasubiri kwa hamu maaamuzi yatakayotokana na taarifa ya Richmond na taarifa ya tume inayoangalia mikataba ya migodi.
    Nashukuru No.3 hapo juu aliyetujulisha kuwa Ndulu hakuwa na Balali wakati uozo unaendelea manake hata mie nilipata wasi wasi sana kusikia naibu wake ndo kapewa kiti.
    Nasubiri pia kwa hamu hatua nyingine muhimu inayohitajika kufuatwa kuangalia msururu wa watoto wa vigogo BOT,hatukatai wanaweza kuweko huko ila wawe na sifa zinazostahili.Lakini pia watoto wa walala hoi wenye sifa wafikiriwe pia.Ni miaka ya hivi karibuni tuu ndio nimeona vacancy za BOT zikitangazwa kwenye magazti ila utasikia fulani yuko BOT ukiangalia Sir name mtoto wa Waziri Mkuu,Mtoto wa Judge fulani,Mtoto wa Waziri fulani,Mtoto wa katibu mkuu fulani,tumesoma nao shule za awali tunawajua.
    Tanzaniadream nasubiri comment zako katika hii issue ya BOT,nilienjoy sana katika issue ya Miss TanzIndia ahaaaa haaaaaa

  10. Comment by micah simons shinshi,UD on January 10th, 2008 2:18 am

    Sasa imedhihirishwa kwamba ukweli ni ukweli na kamwe hauwezi kuwa uwongo. Ivi Si hawa hawa viongozi wakuu wa serikali ndio walikuwa wa kwanza kumpinga Dr SLAA kwa tuhuma hizi hizi. Sasa leo atasema nini SPIKA SITTA akipewa nafasi ya kujitetea kua si mtetea uovu ambaye alikua akikunja ndita bungeni kumpinga Dr SLAA kwa tuhuma hizo. Atasema nini waziri mkuu,meghji na wabunge wa CCM waliokua wakipinga ukweli.
    HOSEA mwenyewe wa TAKUKURU ndiye mficha mauvu kwani alitoa taarifa kuitetea RICHMOND ambayo leo imeundiwa TUME kuichunguza upya wala hafai,au kwa kua kuna wakubwa wanahusika?. Eb sasa tubadilike na tubadili miundo ya utendaji inayompa mtu uwezo wa kutohojiwa kwa uovu.’lets change for changes.

  11. Comment by Kekue on January 10th, 2008 7:17 am

    Heri ya mwaka mpya bc wote!! Mimi simpi hongera kwa kumchagua Ndulu!! Nampa hongera kwa kumwachisha kazi Balali. Kwa sababu jk kumteua naibu wa Balali kuwa Balali mwenyewe wakati yeye ndo alikuwa naibu wa Balali nashangaa sn! kama Gavana hayupo naibu ndo anashika nafasi ya Gavana au siyo? ina maana kwamba wakati balali hayupo Ndulu ndo alikuwa anachukua nafasi ya Balali!!!! au aliyokuwa akifanya Balali Ndulu alikua hayajui mh!! Mimi hainingii akilini kabsaaaaaaaaa!!!! Tz dream sijui yuko wapi na Maty, Ndaki nimeshamsikia.

  12. Comment by kijiwe on January 10th, 2008 11:06 am

    kamwe vasco hatoweza kumfunga balali sababu he belongs to the system remember huwezi kucompare kifo(balali) na usingizi(vasco).
    big up majita for that comment thats a deep one! I SALUTE you for that

  13. Comment by queen on January 10th, 2008 4:09 pm

    Ninakupongeza muheshimiwa raisi kwa matamko yako ,imenionyesha vile ulivyokasirishwa na mafisadi,wabinafsi hawa wasiopenda maendeleo ya nchi yao.Hao ni mwanzo,mbona nchi yetu imeozaa kwa wizi! Ninakuomba usicheke na kima, wala usiangalie makunyanzi wewe wajibika kwa sheria sio kumwonea haya mtu.wawajibishwe kwa sheria bila kujali alikuwa nani au ni nani.Hapo tutajua kweli tunae rais wa wote na sio wa akina fulani.Onyesha mageuzi baba tuponyuma yako tunakuombea afya, usalama na utulivu.Ile sera ya kubebana hakikisha unaivunja hapo utakuwa umeshinda kwa kishindo kwa faida ya Taifa nzima na sio kwa wachache kama inavyoeleweka.Kaza buti baba nchi yetu ni masikini lakini baadhi ya wananchi ni matajiri kupindukia. na mali zao zimefichwa nchi za nnje.

  14. Comment by Msukuma wa shy on January 10th, 2008 6:15 pm

    Sina cha kumpongeza kiwete wala nini,Nampongeza Dr Slaa aliyetupa habari hii ya ufisadi wa BOT.Huyu Dagama anatufanya sisi ni puyuyu!!Eti kamwachisha kazi Dalali,Mtu Dalali mwenyewe alishajiuzulu tangu mwaka jana,hii yote ni kutulaghai wadanganyika ili tumuone ni Rahisi mwenye uadilifu ili tumpe kura mwaka 2010 na vile ameona imebaki miaka miwili tu ndo anajidai kuonyesha makali yasiyo na kichwa wala miguu.

    Ntakupa pongezi tu endapo utatuma watu huko USA wamkamate huyu Dalali aletwe Ukonga au segerea au alipe hizo pesa la sivo wamfilisi mali zake zote abaki matako meupeeeeeeee.Then walioshirikiana nae kulipa pesa hewa kwenye hayo makampuni najua humo wamo mawaziri wakubwa wa nchi nao wawajibishwe kwa kulipa au kufilisiwa mali zao na wakishindwa wakaungane segerea na kina Kasusura .

    Kazi kutuibia madini yetu shy na hata mkoa hamuupi thamani hata kdg yaani buzwagi,mwadui,bulyanhulu yote haya machimbo yapo shy na yanaliingizia taifa mabilioni ya shilingi zinazoishia kugawanwa na wanene wa nchi,hamkumbuki hata kujenga barabara kuwanufaisha wasukuma wenzangu looo.
    niishie hapa nisije andika kisukuma bure kwa hasira.

  15. Comment by lily on January 11th, 2008 12:33 am

    Kumpa naibu Gavana kiti hapo JK hapo mzee umechemsha. yeye ndiye alikuwa mshauri mkuu .alitakiwa aletewe boss mpya wa Kufichua mambo. maana nasikia akaunti zilizoibiwa ni nyingi sana .

  16. Comment by Matty on January 11th, 2008 5:50 am

    Kekuu heri ya Mwaka mpya na wewe! mimi kwa kuwa simfahamu sana huyo Ndulu nashindwa nisemeje ila mama wa Kichaga ashatupa info kuwa Naibu wake (Bukuku) ni mtu makini sawa tunasubiri kuona matokeo maana watakuwa wanashauriana, mimi naona kama BOT imeshaanza kusafishwa basi panga liwe na makali heavy likate kila mhusika wa ubadhirifu wa hayo mabillions na lazima Balali alikuwa na washirika wake pale pale bot na wengine wapo serikalini katika systeam nyeti hivyo ni bora kamanda Tosy afanye msako mkali huko msituni (usa) ili jamaa afikishwe mbele ya sheria.
    Kumfukuza job tu haitoshi maana hajakomolewa wala nini anaomshiko wakutosha kuishi maisha ya starehe mpaka kufa.
    Wale watoto wa vigogo walioko BOT jamani ni kweli wanafit pale kielimu au ndo mambo ya undugulaization??

  17. Comment by John. on January 11th, 2008 7:32 am

    Sioni sababu ya kumpongeza J.K. Kwa sababu kilichofanyika hapo ni “Funika Kombe mwanaharamu apite”Kwa sababu hizo Pesa hakula Balali peke yake, amekula na Vigogo wa Nchi ambao wananyadhifa kubwa tu serikalini pamoja na wafanya Biashara wao waliokuwa wanachangia mamilioni kwenye kampeni za C.C.M(Walikuwa wanalipa Fadhila).Sasa Balali atakapofikishwa kwa Pilato hatokubali kufa kibudu,kwa hiyo lazima sirikali imlinde huko alipo kwa ghrama yeyote ile,ili asitoe siri.Kama mnabisha mtaona BIlali atajiuguza huko Marekani hata Miaka Kumi.Wapo wapi Akina MATAKA former Boss of PPF ,Ipo wapi Kesi ya Dito?Wakati Kesi ya Babu Seya mwaka haikuchukua mtu kala Mvua.Ipo wapi kesi ya Mahalu?Ipo wapi kesi ya Misambano ya Kubaka?hivyo ndivyo system inavyofanya kazi.Hata wakishitakiwa hizo kesi zitachukua hata miaka ishirini Kuisha.Usitegemee haki Duniani haki ipo kwa Mungu.Na ndio maana mtu akifa kuna msemo Maarufu-”Ametangulia mbele ya haki”kwa maana hapa Duniani Hakuna Haki.Let’s wait and see Time will tell.
    John.

  18. Comment by Kekue on January 11th, 2008 7:52 am

    Matty kumtoa balali na kumuweka naibu wake jk kachemka, hivi c kuna uchunguzi unaendelea huyo Ndulu akibainika kuwa nae yumo? yani hapa jk asingemchagua mtu kutoka huko bot kabisa angemtoa sehemu nyingine, naungana na Lily hamuwezi kuwa Gavana na naibu wake mmoja afanye kitu mwenzie asijue!! Si wangeshaparangana??? lazima walikuwa wanashauriana na kushirikiana. He!!!

    Na huyo Balali sijui dalali arudishwe hapa aje ataje wenzake na kufilisiwa kufuate mara moja ili hizo pesa zipunguze hayo mabilioni hapo jk kidogo atakuwa ameonyesha kasi na nguvu mpya, na wenzake wote dawa hapa ni kufilisiwa kila kitu, sio kumfukuza kazi alafu aende akaishi na familia yake USA. Yani asiporudishwa hapa jk hapo ni sawa na kamstaafisha na mafao yake yote kapata. He wajameni hizo pesa ni nyingi mno!!!! Jk atath***tuuuu???????????????????????

  19. Comment by NYAU on January 11th, 2008 9:47 am

    Majita hiyo IFM u mean Institute of Finance Management or IMF? hah

  20. Comment by jobiii1 on January 11th, 2008 4:23 pm

    Watu wanapupa ya kusema bila kuelewa. Ndulu amekuwa naibu BOT chini ya Mwezi mmoja. Juma Reli ndiye aliyekuwa deputy siku zote. Get your facts right kabla ya kumlaumu JK.

  21. Comment by Majita on January 11th, 2008 6:13 pm

    Jamani Nyau wasu.
    Yani hizi shida za huku Majita lazima nitachanganyikiwa tuuu na Maisha.Unacheza nini na ugali wa mhogo kwa maembe ya kupikwa.Nilikuwa namaanisha ile ya rafiki yake baba wa Taifa aliyokuwa anaingolea sana kwenye mikutano yake.Ile ya ya ya INTANESHINO MONETARI FANDI,si ndiyo IFM au kuna utofauti.Si unajua tena na ushamba ndg yangu.Ila simaanishi chuo cha usimamizi wa fedha.Kazi ipo.

    Ndg Jobii watu hawakurupuki bwana kuongea.Anaekurupuka ni wewe,Spika ndg 6 na PM EL kwani nyie ndo mlikuwa mnataka kumshitaki Dr “SIRAHA” ya maangamizi kwa kutoa ushahidi feki wa BOT.Upo hapo???
    Sasa hata kama Mr.Juma Reli ndo alikuwa Naibu wa Balali kwa muda mrefu wewe umesikia amefanyiwa nini.Au nae kaondolewa hapo BOT??? acha bwana.WATU WANA USHAHIDI NA WANAWEZA KUKUPA IDADI YA MAJINA YA VIGOGO WALIOPATA HUO MGAO NA KIASI CHA HELA KWA KILA KIGOGO.

    Ndg Jobiii kumbuka kuwa makampuni mengi yaliyokwiba hela zetu hapo BOT yalifunguliwa mwishoni mwishoni mwa utawala wa balali & huyo ndg yako Ndulu akiwa ndani ya nyumba.

    Dedication-mwimbo wa Banana Zolo wa “Byotii”

    …Vipi kuhusu Buzwangi,yule binti wa Madini,acha yule “Byotii” mwenye mtoto wakoooo! Balali hazai peke yake,lazima kuna mwanamke (Msamehe) kuhusu huyo twini tawa twini twawa wa wengiiiiine.Mbona kigugumiziii…..
    © Majita

  22. Comment by Kekue on January 12th, 2008 2:18 am

    Majita aminia!!!!!!!!!!

  23. Comment by Matty on January 12th, 2008 3:11 am

    Majita nimependa hako kasongi hapo chini kanatia hamasa sana ya kujua umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu (dhati iz why balali sijui dalali wa nyumba hakuwa isolated wakati wa kutake chake mapema.
    Leo nimesikia na Patel tayari yumo kwenye hilo zengwe la BOT safi sana tunataka wote na sio kuwataja tu…pls rais wapelekwe njia panda ya segera(segerea) na united kingdom (ukonga) ili wajue watu hawataki upuuzi na nchi yao, wapinzani walivyokuwa wanalalama watu waliwaona wamechanganyikiwa leo aibu imewakuta PM, spika na wenzake.

  24. Comment by Rodney on January 13th, 2008 10:41 am

    Ok. Kazi nzuri na walioteuliwa wanafaa kabisa. Kama Prof. Ndulu Muda mrefu alikuwa World Bank kwa hiyo ana uzoefu wa kimataifa. Sasa tunahitaji JK atwambie nini kitafuata kwa Balali na waliohusika kwani kumtimua tu haitosho inapaswa atiwe kizuzini na sheria ifanye kazi yake…..

    Mdau Sweden nikisaka nondo.

  25. Comment by shally on January 16th, 2008 3:57 am

    hivi beno hataiba kweli au yeye hapendagi hela maana wabongo tunajuana tunamshangaa balal but all we are the same

  26. Comment by julie on January 21st, 2008 2:45 am

    Meghji yumo kwanini akubali kudanganywa na Ballali? kwanini hakumuuliza katibu wake Mkuu, ambae ni muadilifu na smart?
    alichukua hatua gani ya kinidhamu alipogundua Ballali ni mwongo na jasusi?
    Mkapa alimtoa wapi huyu mwizi? ndie alimpa kichwa?

Leave a Reply