MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

Sekta ya burudani nchini Tanzania imekuwa ikipitia mabadiliko mwaka hadi mwaka,siku hadi siku. Kuna wakati burudani ya disko ndio ilishika hatamu.Hii ilienda sambamba na sinema,zile za yale majumba ya sinema ya enzi zile.Hapa nazungumzia kina Drive Inn Cinema,New Chox,Empress na wenzao. Kisha kuna wakati taarabu ikaja juu.Ukawa ni mwendo wa “mipasho”.Kina Nasma na Bi.Khadija wakawa ndio gumzo la mjini. Haukupita muda muziki wa kizazi kipya ukashika hatamu.Bongo Flava ikawa ndio ya kuamkia na ndio ya kulalia.

 

 

Lakini kabla Bongo Fleva haijapotea (bado inatamba) enzi za filamu za kitanzania,zenye lugha yetu wenyewe,waigizaji wetu wenyewe,zikarejea upya. Hivi sasa Bongo Fleva na Filamu za Kitanzania zinabakia kuwa burudani za aina yake nchini Tanzania. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba filamu za kitanzania zina historia ndefu.Tangu enzi zile za kina Fimbo ya Mnyonge,YombaYomba,Harusi ya Mariam nk. Kinachofanyika hivi sasa ni kurejesha enzi zile.

 

Mtu mmoja ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa kuzirudisha zama zile za filamu za kitanzania ni Sultan Tamba ambaye ni mtunzi wa hadithi,mwandishi wa magazetini na vitabuni na pia muongoza filamu. Filamu yake ya iliyoitwa Girlfriend ya mwaka 2002 ambayo aliwashirikisha wasanii kama T.I.D, kundi la East Coast na baadhi ya wacheza filamu walio maarufu sasa kama Monalisa na wengineo, ilichangia sana kuamsha upya ari ya kutengeneza tena filamu za kitanzania.Wakati huo filamu za kutoka nchini Nigeria zilikuwa zishaanza kuotesha mizizi miongoni mwa wapenda filamu nchini Tanzania.Mpaka hivi leo bado zinapendwa nchini Tanzania ingawa hivi sasa zinakumbana na ushindani mpya wa filamu za kitanzania.

 

Hivi karibuni tulifanya naye mahojiano na Sultan Tamba ambapo tumezungumzia mambo mengi kuhusiana na kazi zake za uandishi,utunzi wa hadithi za filamu,uongozaji filamu na mengineyo.

 

Muhimu zaidi alitueleza juu ya ujio wa filamu yake mpya ambayo ameiita Soka la Bongo.Filamu hiyo inatarajiwa kutoka takribani wiki tatu zijazo.Inahusu nini?Kwanini ameiita Soka la Bongo? Unawajua top six wake kwa upande wa waigizaji filamu nchini Tanzania?Ana maoni gani kuhusu wanamuziki kugeuka kuwa waigizaji? Anasemaje kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania? Upo? Unajua ameanza kuandika tangu akiwa na umri gani? Kwa hayo na mengineyo mengi fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

 

BC: Kwanza naomba uniambie historia ya maisha yako kwa kifupi.Ulizaliwa wapi,ukasomea wapi na mambo kama hayo.

 

ST:Nilizaliwa Dar es Salaam, Ilala mwaka 1973, nilisomea shule ya msingi inayoitwa Ilala Boma, iliyopo jirani kabisa na ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Sakaam. Nilipomaliza darasa la saba niliendelea na sekondari hadi kidato cha pili, halafu sikuweza kuendelea tena kutokana na uwezo wa kifedha wa kifamilia kuwa chini, Huo ulikuwa ni mwaka 1991

 

Nikajiingiza kwenye mambo ya uchoraji kwenye magazeti, kuanzia gazeti la Uhuru na magazeti ya Cheka na Wasaa, kisha kuanzia hapo nikajikuta naweza mambo mengi ya magazeti na nikaendelea mpaka hivi sasa. Hapo katikati nikawa najiendeleza kwa kuchukua kozi mbalimbali katika mambo ya habari na mawasiliano na pia za kiingereza.

 

BC: Unatoka kwenye familia ya watoto wangapi?

 

ST: Natokea kwenye familia ya watoto 11 lakini saba tuko baba mmoja mama mmoja. Wengine baba alizaa na wake wengine.

 

BC: Ulipokuwa mdogo unakumbuka ulitaka kuwa nani ukubwani?Na unakumbuka nini zaidi kuhusu maisha yako ya utotoni

 

ST: Nilitamani sana kuwa mwandishi.Utotoni nakumbuka zaidi nilivyokuwa napenda kujifungia chumbani nikiwa na lundo la makaratasi yangu niliyokuwa nayanunua sokoni.

 

BC: Ulikuwa ukijifungia unaandika au kuchorachora tu wakati huo.

 

ST:Kwanza sikumbuki ni lini nimejua kusoma. tangu nilipoanza nursery school, mwaka wa kwanza tu nilikuwa najua kusoma na kuandika kwa vizuri sana kiasi barua za mechi za timu za mitaa yetu yote nilikuwa naletewa mimi. Nilikuwa najifungia kuandika hadithi, nyimbo ninazozisikia na kujichorea picha mbalimbali katika vijitabu nilivyokuwa natunga tunga mwenyewe tu wakati huo.

 

BC: Unaweza kukumbuka nani hasa alikuvutia kwenye masuala hayo ya uandishi na usomaji? Nauliza hivyo kwa sababu watoto wengi kwenye umri huo wanapenda zaidi kucheza chandimu na michezo mingine kama gololi nk.

 

ST: Wakati ule nilivutiwa sana na michoro ya Phillip Ndunguru kwenye gazeti la Sani, na nikawa naiga anavyochora na kisha natunga watu wangu. Lakini sikuacha mpira, nilicheza kama watoto wengine, ila zaidi nilionekana nafuatilia sana kutunga hadithi, kuandika vitabu, kuchora na kuandika nyimbo ninazosikia. Mara nyingi nilitumia muda wangu kwa mambo hayo.

 

BC: Unakumbuka ni lini mchoro wako au hadithi yako ilichapwa gazetini kwa mara ya kwanza?Ilikuwa gazeti gani?

 

ST: Nakumbuka ilikuwa ni barua ya uchambuzi kuhusu swali fulani la watoto kwenye gazeti la Uhuru mwaka 1987, nikiwa darasa la tatu. Halafu mchoro wangu wa kwanza ulichapishwa na gazeti lililoitwa CHEKA mwaka 1990 na hadithi yangu ya kwanza ilichapishwa na gazeti la WASAA mwaka 1991.Iliitwa Penzi la Tapeli.

 

Labda niongezee tu kwamba, kutokana na uchoraji, uandishi na utungaji mashairi niliokuwa nikiufanya wakati huo, baadhi ya waandishi wakongwe walivutiwa na mimi na wakaniona nina kipaji jambo ambalo lilipelekea wao kunijumuisha katika kikundi cha waandishi 7 kutoka Tanzania walioalikwa kuwa na mazungumzo na waandishi wa Finland nyumbani kwa balozi wao kule Sea View.

 

Katika msafara ule nikawa mtoto peke yangu, na aliyejitoa nafasi yake niichukue mimi alikuwa ni Hammie Rajab. Alisema anapenda mimi niwe kama yeye, akajitoa na nikaenda mimi. Kiongozi wetu katika mkutano ule alikuwa ni Ndesumbuka Merinyo – sasa ni mkurugenzi wa duka la Afrika Sana. Wengine niliohudhuria pamoja nao ni Kajubi Mukajanga na wengine ambao kwa utoto wangu siwakumbuki vizuri.

 

BC: Historia ya maisha yako inaonyesha kwamba umekuwa ukijishughulisha kwa namna nyingi katika uandishi wa magazetini. Ulijiunga lini rasmi na magazeti? Ilikuwa ni gazeti gani?

 

ST: Nilijiunga rasmi na magazeti mwaka 1990 na hapohapo nikaingizwa kwenye chama cha waandishi wa vitabu kilichokuwa chini ya K.M. Kassam, Ben Mtobwa, Kajubi Mukajanga, Hammie Rajab na wenzao waliokuwa maarufu wakati ule, japo sikuwa na kitabu hata kimoja bali hadithi kadha wa kadha tu.

 

BC: Toka mwaka huo wa 1990 umekuwa na vyombo vipi vya habari au magazeti gani?Na ilikuwa liniulipoanzisha gazeti lako mwenyewe?

 

ST: Nilifanya kazi magazeti mengi yaliyokuwa yanazaliwa wakati huo. Kimsingi miaka hiyo magazeti yalikua ni Uhuru, Mzalendo, Mfanyakazi na Kiongozi.Lakini baadae yakaanza kuchipuka Motomoto, Cheka na Wasaa, mimi nilianza na Cheka na Wasaa – baadae yalizaliwa Heko, Wakati ni Huu, Busara na 1994 likaanzishwa Majira ambalo pia nilifanya kazi. Nilisajili gazeti langu mwenyewe mwaka 1994. Kimsingi karibu kila gazeti lililozaliwa wakati ule na mimi nilichukuliwa kusaidia kuandika.

 

BC: Ni gazeti gani hilo ulilolisajili mwaka 1994?Lipo hai bado?

 

ST: Linaitwa Shangwe. halijafutwa na serikali, limo kwenye orodha ya magazeti nchini japo halichapishwi kwa sasa. Lilitoka kwa awamu mbili, kipindi cha uchaguzi wa 1995 hadi likakoma mwaka 1997 kisha likaibuka tena mwaka 1998 likasimama 2000.

 

Sultan Tamba akiwa ofisini kwake

 

BC: Ni changamoto gani ambazo umekumbana nazo na gazeti lako la Shangwe?Unadhani kwanini halijasimama imara?

 

ST:Kilichokwamisha lile gazeti ni mtaji.Limekuwa likianzishwa kwa mitaji midogo chini yangu mwenyewe na hivyo kukwama baada ya mwaka au zaidi. Ila kwa kuwa nimeshaongoza magazeti mengi hadi sasa, nimejifunza mengi zaidi na litachapishwa tena, ndiyo mipango niliyonayo.

 

BC: Unaliongelea vipi suala la uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania?Upo?Kwa kiasi gani?Unatosha?

 

ST:Uhuru wa vyombo vya habari upo kiasi. Lakini hautoshi kwa sababu serikali imekuwa macho sana na masuala ya siasa.Wanahisi kwamba magazeti mengi yanatumiwa, kwa hiyo kubanwa hasa kwa magazeti yanayoandika siasa ndiyo maisha yenyewe na wapo waandishi ambao wanapata usumbufu mkubwa zaidi. Kama ukiwa na gazeti la mitaani, haya yanayoitwa ya Udaku, usumbufu si mkubwa, ila wenye magazeti ya siasa nadhani uhuru wao ni nusu. Niliwahi kushiriki huko nyuma magazeti hayo na hata langu liliwahi kuwa gazeti la siasa na mengi yalitutokea.

 

Kwa mfano nakumbuka Cheka lilivyofungiwa nikiwa ni mmoja wa waandishi wake mwaka 1993. Kama sikosei ndio gazeti la kwanza kwa serikali kutangaza kulifuta kabisa. Kisha MICHAPO, nalo lilifutwa na serikali nikiwa ni miongoni mwa wachangiaji wa gazeti hilo. Haya yalishughulika na siasa kwa kiasi kikubwa sana.Halafu angalia namna serikali inavyodhibiti magazeti, mweka hazina wa CCM Rostam Aziz (alikuwa) amenunua gazeti la Rai lililokuwa linaongoza kwa kuchapisha habari za kuikosoa serikali ya CCM, akabadilisha na policy ya gazeti kuwa ni ya kichama. Hivi sasa ndio maana unaona akina Ulimwengu waliokuwa kwenye gazeti hilo wamejitoa na wameanzisha lingine hili linaloitwa Raia Mwema ambalo limeanza kutoka hivi majuzi.

 

Kimsingi ukitaka kuepuka matatizo na pengine uone uhuru wa habari unatosha, basi gazeti lako lielekeze liwe linawasaidia CCM kinyume cha hapo utakumbana na misukosuko, iwe ya siri au dhahiri.

 

BC: Hivi sasa unaandikia gazeti gani? Linatoka mara ngapi kwa wiki?

 

ST: Kwa miaka mitatu mfululizo nilikuwa Mhariri wa gazeti la Sani (lilelile ambalo utotoni nilikuwa naigiza michoro yake) halafu mwaka jana nikapumzika, mwaka huu nimechukuliwa kama miongoni mwa wahariri wa gazeti la Kiu, linatoka mara mbili kwa wiki Jumatatu na Ijumaa.

 

BC: Kwa mtazamo na maoni yako,nini mchango wa magazeti ya Udaku(tabloids)katika kujenga au kubomoa maadili ya kijamii hususani kwenye nchi za kiafrika kama Tanzania?

 

ST: Magazeti ya Udaku yaliyo mengi yanabomoa maadili – mabosi wake huzama zaidi katika kufanya biashara kuliko huduma ya habari. Jambo hilo limesababisha wahariri wengi kuandika chochote kinachouza bila kuangalia upande wa pili na ili mradi gazeti linauzika mabosi wako tayari kutetea. Kadhalika wahariri wengi wa magazeti haya si wasomi na mabosi pia hawawataki waandishi wasomi kwa kuwa watapingana nao na matokeo yake gazeti halitauzika. Wengi wa wahariri ni vijana sana wasio na uzoefu wowote katika masuala ya habari. Unaweza usiamini lakini ndio ilivyo.Kwa upande mwingine ni magazeti ya burudani zaidi, hadithi na ucheshi, lakini sura za mbele za magazeti yetu haya, binafsi si kwa manufaa ya wasomaji, ni kwa manufaa ya wenyewe.

 

BC: Kwa hiyo unashauri nini kifanyike?

 

ST: Nafikiri ni wanahabari wenyewe, Baraza la Habari na Taasisi zingine zisaidie katika uanzishwaji wa kozi hata kama ni fupi fupi za kuwanoa waandishi kwa gharama nafuu kwani inaeleweka masomo ya uandishi ni ghali sana.

 

BC: Okay,mbali na uandishi wa magazetini,wewe pia ni mtunzi mzuri wa hadithi za vitabuni.Mpaka hivi sasa umeshaandika vitabu vingapi?Unaweza kuvitaja kwa majina?

 

ST: Nimeandika kama vinne au vitano hivi lakini ninavyokumbuka zaidi na vilivyotokea kupendwa zaidi ni Mambo ya Fedha, Shetani wa Mahaba na Mzee wa Busara.

 

BC: Hivi vyote vimechapwa na kampuni gani?

 

ST: Yangu mwenyewe, Sultan Company na Tamba General Enterprises LTD

 

BC: Watu wengi ambao ni waandishi au wanaweza kuwa waandishi wa vitabu hawafanyi hivyo kwa sababu wanasema soko la vitabu ni duni kwa sababu watanzania hatuna mazoea au mapenzi ya kujisomea.Je unadhani dhana hii ina ukweli?Na kama ndio,nini basi kifanyike ili kurekebisha hali hii?

 

ST: Inategemea na vitabu vyenyewe.Mara nyingi vitabu vya hadithi ninavyojua mimi, vina soko zuri kama utavitangaza au vitakuwa na hadithi nzuri na watu wakaipenda na kuambiana au pia umaarufu wa mwandishi mwenyewe unaweza kusaidia. Mara nyingi hadithi huwa zina wapenzi wengi.Hii ni tangu zamani kipindi kile cha wakongwe Hammie Rajab, Kajubi, Musiba na wenzao.

 

Lakini vitabu vya aina nyingine, labda vya kuhusu elimu fulani, pengine upishi, uvuvi au vyovyote vya kielimu, ukataka kuuza mtaani, hapo kunakuwa na tatizo la soko.Labda kama vitabu hivyo vitakuwa ni kwa ajili ya mashule, soko litakuwa huko. Mitaani wanunuzi ni watu wa kawaida ambao wana mtazamo mwepesi katika kusoma magazeti na vitabu.

 

BC: Kwa maana hiyo unachotaka kusema ni kwamba waandishi wajitokeze tu,waandike vitabu vizuri kuendana na hadhira,soko lipo.

 

ST: Hiyo ni kweli. Ila ni lazima wavitangaze. Soko lipo. Bila kutangaza ni vigumu kwa kweli kuuza vitabu.

 

BC: Mojawapo ya vitabu vyako nasikia vinatumika katika shule ya msingi.Hongera sana kwa hilo.Ni kitabu gani hicho na ilikuwaje kikaingizwa mashuleni?

 

ST: Ni Mzee wa Busara. Kiliingizwa katika mpango maalum wa vitabu vya ziada.

 

BC: Kwa maana hiyo ni non-academic book.

 

ST: Ni hivyo.

 

Pichani ni Joseph Kaniki (aliyeshika gazeti) na JB(pembeni yake) wakiwa chini ya uongozi wa Sultan Tamba wakati wa kutengeneza movie ya Soka la Bongo inayotarajiwa kutoka hivi karibuni.

 

BC: Sasa tuje kwenye upande wa filamu.Ilikuwaje ukajiingiza kwenye masuala ya filamu? Nini kilikuvutia.

 

ST: Nilitamani filamu tangu mdogo, na nilivutiwa na sinema za kizungu. Halafu mwaka 2002 nilihamasika zaidi kutokana na filamu za Nigeria kuingia kwa wingi hapa kwetu na kutufunika. Iliniuma kidogo na ndiyo nikahamasishwa kutunga sinema yangu iliyoitwa Girlfriend na kuanzia hapo hamasa ikapatikana.

 

BC: Filamu yako ya Girlfriend ndio inasemekana ilirejesha upya hamasa ya filamu nchini Tanzania ambayo ilikuwa imepotea kwa muda toka enzi za Fimbo ya Mnyonge,YombaYomba nk.Ulitunga tu hadithi ile au ilikuwa ni kisa cha kweli?Nani aliongoza filamu ile?

 

ST: Ni kweli, ilipandisha hamasa. Haikuwa kisa cha kweli, nilibuni tu. Kimsingi nilikuwa na lengo hilo la kukuza hamasa, kwa hiyo nilitumia muziki wa bongo fleva ambao kipindi kile ndio ulikuwa juu sana.Nikawatumia wasanii wa bongo fleva waigize filamu na kuingiza nyimbo zao zilizopendwa sana kipindi kile.Lengo lilikuwa ni kuwavuta wale waliochanganyikiwa na bongo fleva kuangalia filamu huku tukiwashtua wapenzi wa filamu kwamba tunaweza kutengeneza kazi zetu kwa vijana maarufu tulionao.Iliongozwa na mkenya- George Tyson.

 

BC: Tangu pale umeshatunga au kutengeneza filamu ngapi?Unaweza kuzitaja?

 

ST: Zinafika 17 au zaidi. Girlfriend, Siri,Bosi, Mzee wa Busara, Shetani wa Mahaba, Noti,Chozi la Damu,Roho Mbili, Jinamizi,Pete, Bestfriend, Miwani Mieusi, Kazibure Village, Kisu, Sumu ya Moyo, In the House na Mzee wa Busara II.Ya mwisho ni hii ninayotarajia kuitoa hivi karibuni inayoitwa Soka la Bongo.

 

BC: Katika zote hizo unadhani ipi ilikuwa ngumu zaidi kuitunga,kuitengenezea script, na katika uigizaji wake.Kwanini?

 

ST: Ni Sumu ya Moyo. Nilijaribu kubadilika hapo, kutengeneza hadithi inayohusu zaidi matatizo ya mila na mfumo dume vijijini. Niliigharamia mwenyewe kila kitu na nilitafuta wasanii wazoefu na niliwafanyia na semina ya siku mbili. Pia nilichukua cameraman mwingine, hivyo ilinisumbua kwa kipindi kirefu cha kuirekodi, gharama zake na ilinilazimisha kuifuata hadithi vile nilivyoitunga japo mara nyingine mazingira yalikataa kuipiga kama nilivyoandika.Pia ilinilazimu kama muongozaji kuhakikisha waigizaji wanafanya vile script ilivyoandikwa kwa hiyo tulichukua muda mrefu na wasanii walichoka sana. Lakini hatimaye ilitoka na ni mojawapo ya kazi zangu nzuri kwa uwezo wangu binafsi.Najivunia hilo.

 

BC: Baadhi ya waigizaji filamu ambao tumeshafanya nao mahojiano wamekuwa wakilalamikia suala la serikali kutowaunga mkono na pia kuwa vigumu kuigiza filamu katika maeneo fulani fulani yaliyo chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa serikali.Unaliongeleaje suala hilo?

 

ST: Ni kweli kabisa kusema kwamba serikali haiungi mkono harakati hizi za filamu japo zina faida nyingi tu kwa serikali na taifa kwa ujumla.Na ni vigumu kweli kuigiza kwenye maeneo fulani na hata kupata msaada wa matumizi ya baadhi ya vitu kama vile sare za polisi au hata magari hata kama sinema yenyewe itaisaidia serikali dhidi ya jambo fulani.

 

Lakini mimi nafikiri bado tunaanza. Haya yanaweza kubadilika. Naamini kadiri ongezeko la utoaji filamu linavyokua na itafika mahali serikali italiona hili na itakuwa na msaada fulani fulani katika hayo tunayoyataka.

 

Kwa sasa tuko karibu na Kaimu Katibu wa Bodi ya Ukaguzi wa filamu iliyo chini ya Wizara ya Habari na Utamaduni.Binafsi amenipa matumaini mengi na anajaribu kusaidia kadiri ya uwezo wake. Nafikiri tutafika, muda bado upo.Safari ni ndefu.

 

BC: Kwa sasa ungependa kutoa ushauri gani kwa serikali?

 

ST: Watusaidie katika kuanzisha kozi mbalimbali za utengenezaji wa filamu. Hii itasaidia walio kwenye fani hii sasa hivi na wanaotaka kuingia kupata pa kuanzia. Gharama za masomo ya filamu ni kubwa katika chuo kikuu, kwa siku ni dola 300! na hakuna chuo chochote cha filamu! Ndio maana watu wanajifanyia tu.

 

BC: Okay tukirudi kwenye suala la uigizaji filamu.Kumekuwepo na tabia ya wasanii wengi wa muziki pia kuwa waigizaji.Utaratibu huu ulipoanza nchini Marekani,wapo watu waliouponda sana wakidai uigizaji ni fani tofauti na muziki.Wewe umeshatumia wasanii wa muziki katika filamu zako.Nini mtazamo wako katika suala hili?

 

ST: Mimi nafikiri kipaji cha uigizaji kipo kwa mtu yoyote. Anaweza kuwa mwanamuziki, lakini akawa na kipaji kignine. Si lazima binadamu kuwa na kipaji kimoja, unaweza kujaaliwa uchoraji halafu hapohapo ukawa na kipaji cha soka na hapohapo ukawa na kipaji cha hesabu shuleni. Vyote vinawezekana.Kadhalika, kipaji ni kitu kilichojificha, hutokiona usoni kwa mtu. Kinaanza kujitokeza kwa mtu mwenyewe kusema NAPENDA KUIGIZA, AU NAPENDA KUIMBA kinachofuata ni kujaribiwa kwamba anapenda tu au ana kipaji?

 

BC: Tukirudi kidogo kwenye hadithi za filamu zako.Kumekuwepo na maoni kwamba hadithi nyingi za filamu zako ni kama vile unaziiba tu kutoka kwa wa-nigeria na kuziweka katika kiswahili.Unasemaje kuhusu shutuma hizo?

 

ST: Si kweli hata kidogo.Tena bahati mbaya kinachonivutia kwenye sinema za Nigeria ni umarufu wake lakini sio filamu kama zilivyo.Mimi napenda sana filamu za kusini mwa Afrika, Zimbabwe, Afrika Kusini na jirani zao, ziko serious kuliko za Nigeria. Sijui hata hadithi moja ya filamu ya Nigeria kichwani mwangu, si mtazamaji wao – ila navutiwa kutaka kujua wamewezaje kufika walipo. Nawaunga mkono kwa kuweza kupata mafanikio, lakini filamu zao zina msururu wa makosa ambayo yanazuilika!

 

BC: Wapenzi wengi wa filamu za Tanzania wamekuwa pia wakilalamika kwamba filamu za kitanzania ni predictable sana.Yaani ukianza tu kuiangalia unajua itaishiaje.Mnafanya nini ili kurekebisha hali hiyo?

 

ST: Ndiyo maana nilisema serikali itusaidie kuanzisha kozi za utengenezaji filamu, ambapo ni pamoja na uandishi wa script.Ukiwa ni mwandishi mzuri wa script, kitu hicho unaweza kukiepuka, ingawa hadithi kama ilivyo ni ngumu kumuamulia mwandishi aandikeje, lakini makosa kama hayo yanaepukika kama kutakuwepo na misasa ya hapa na pale.

 

BC: Kama mtunzi na muongoza filamu nchini Tanzania,nikikupa nafasi ya kunitajia waigizaji bora watatu wa kike na watatu wa kiume nchini Tanzania hivi sasa ungewataja kina nani?

 

ST: Single Mtambalike anajiita Richie, kuna msanii anaitwa Haji, aliigiza filamu ya masaa 24 na Jacob Labia, ni msanii wa filamu zangu. Hao ni wanaume. Kwa upande wa wanawake navutiwa n Bi Terry wa kundi la Kaole, Monalisa na Zubeda Masanyiwa aliyeigiza filamu ya Jinamizi.

 

BC: Kwa hiyo kwa ujumla unaonaje jinsi soko la filamu nchini Tanzania linavyokua?Unapata matumaini gani unapoona hivyo?

 

ST:Matumaini ni makubwa. napenda filamu, kwa hiyo napenda kuona mafanikio ya kitu hicho yako hapa Tanzania. Bila shaka wawekezaji na makampuni makubwa yatakuja hapa kama tukiongeza bidii na tutapanua ajira yetu na matatizo mengi kwenye fani hii hapa nyumbani yatayapungua. Tutakuwa tunaangalia mambo yetu wenyewe na kujifunza mengi.

 

BC: Hivi karibuni unatarajia kutoa filamu mpya ambayo umeiita Soka la Bongo.Unaweza kutuambia kwa kifupi tu filamu hii itahusu nini na lini itaingia mitaani rasmi?

 

ST:Filamu hii inahusu soka na maisha nje ya soka. Kimsingi tunaangalia tangu changamoto ya Rais Kikwete ya kuamsha ari ya soka Tanzania.Kuanzia pale na mpaka hapa tulipo, kadhalika nimehusisha na mechi zile ambazo timu yetu ilicheza kuwania nafasi ya kwenda Ghana, walioshiriki ni wanasoka wenyewe kama vile Ivo Mapunda, Juma Kaseja,Joseph Kaniki na wengineo.Itatoka wiki tatu zijazo.

 

 

BC: Hivi karibuni ulikwenda nchini Afrika Kusini..ulikwenda kujifunza nini?

 

ST: Nilitaka kusoma mambo ya filamu pamoja na biashara na kujifunza zaidi kuhusu mazingira ya kazi za filamu. Lakini sikufanikiwa sana kwani gharama za masomo ni kubwa, niliweza tu kuona baadhi ya kazi za utengenezaji filamu.Sijakata tamaa nitaenda tena kwa lengo hilo nikijiandaa vizuri.

 

Ivo Mapunda(Tanzania One) katika set ya Soka la Bongo,filamu mpya ya Sultan Tamba.

 

BC: Mwisho unatoa ushauri gani kwa vijana wanaotaka kujiingiza kwenye mambo ya filamu?

 

ST: Nawakaribisha, ila tujitahidi wakati huu ambapo masomo ya filamu Tanzania hayapo, tuwe wasikivu kwa waliosoma na tuwe tunashauriana na kuangalia kazi za wenzetu, tujifunze makosa yetu na tuwe wazi kupokea ushauri na kukosolewa.

 

BC: Kwa upande wa familia..umeoa? Kama ndio una watoto wangapi?

 

ST: Sijaoa ila nina mtoto mmoja ninayetamani awe juu yangu kwa vipaji. Nimemwita TAJI . Si unajua maana ya taji?Ni kile kitu anachovaa SULTANI kichwani!!!!

 

BC: Ahsante sana Sultan kwa muda wako.Tunakutakia kila la kheri katika shughuli zako.

 

ST: Asanteni na nyie pia.Kazi njema.

Share and Enjoy:
  • Digg
  • Sphinn
  • del.icio.us
  • Facebook
  • Mixx
  • Google Bookmarks
  • email
  • LinkedIn
  • Live
  • Spurl
  • Technorati
  • Yahoo! Buzz
  • YahooMyWeb

Feedback / Comments

10 Responses to “KWA KINA NA SULTAN TAMBA.”

  1. Comment by Tarimba on November 8th, 2007 9:48 am

    Mahojiano mazuri.Sultan ameonyesha kukomaa kimawazo aliposema wazi kwamba elimu zaidi inahitajika kwa waandishi na watengeneza filamu.Kila la kheri Sultan.

  2. Comment by gasto on November 8th, 2007 5:14 pm

    Tamba huyu ndo yule sangoma ama?

  3. Comment by Dinah on November 11th, 2007 3:40 am

    Mahojiano mazuri, nimefurahishwa na uwazi wako :-)

    Ila bwana Tamba huoni kuwa kwa “waandishi” wa udaku wakisoma na kuwa na taaluma ya uaandishi wa habari (za maana ktk jamii) hakutakuwa na maana ya udaku?

    Udaku ni umbeya….kuzungumzia, fuatilia mambo na maisha binafsi ya watu(ambayo hayakuhusu) na kufanya hivyo huitaji kusoma bali uwezo na muda wa kufuatilia mambo hayo.

    Kama ilivyo tofauti kati ya “waandishi wa habari wapiga picha” na “paparazi” (wadaku wa picha).

    Kila lililo jema ktk shughuli zako.

  4. Comment by hombiz on November 11th, 2007 3:56 pm

    Fanya kila jitihada ulejee shule ndugu Sultani. Kwa tathmini yangu ya haraka haraka,nimebaini kuwa ukiongeza elimu ktk mambo haya ya uandishi na sanaa ya filamu na uigizaji kwa ujumla, unaweza kuwa mmoja wa wazee wa fani hii wanaothaminika sana barani Afrika na Dunia kwa ujumla. Kipaji unacho. Kiendeleke kaka.
    Kila la kheri ktk kazi zako.

  5. Comment by zaina seif on May 20th, 2008 2:01 pm

    mahojiano mazuri sultan na kazi yako wow! ila me ninaushauri kuhusu movies mnazo tengeneza ingekuwa vizuri wacezaji [waigizaji] wangekuwa wamesomea kazi hiyo. kwa sababu wengi wao huwa wanaharibu kimavazi na hata ucezaji pia! inakuwa kama wanajitahidi kuiga sana, kwa kifupi waelimishwe na pia waongozaji na wasimamizi wawe makini wanapo kuwa wanatengeneza movie. kwa sababu wakati mwingine mnawaweka watu kwenye movie kwa sababu ya umaharufu wao 2 na sio waigizaji wazuri kabisa. big up sultan kheri na baraka kwenye kazi yako

  6. Comment by maryciana on May 20th, 2008 2:47 pm

    we zaina seif..eti ‘wacezaji’ .. ‘ucezaji’ ni kwamba hujui spelling za kiswahili au ndio kiswangrish?

  7. Comment by hans on May 29th, 2008 4:36 pm

    nasoma sana hadithi zako kaka, na kuna kupindi tuliwasiliana kuhusu kutumia hadithi nyingi na mambo ya kishirikina na ulinijibu, lakini kwa kusoma mahojiano haya nimekuelewa na nakupongeza sana. kikubwa ni kukazania sana urudi shule kutokana na hii interview nimeona wengi tuna matatizo na elimu, hivyo kama inawezekana jikusanye vizuri uende tena south africa kusomea mambo ya filamu kiundani, nina uhakika miaka michache ijayo utakuwa mtu muhimu sana nchi ktk sekta ya filamu. big up ndugu yangu

  8. Comment by masai,MD on May 11th, 2009 6:46 am

    elimu ni muhimu jitahidi ujiendeleze

  9. Comment by Peter Tarimo on October 10th, 2009 2:36 pm

    Nakupongeza sana kwa uwazi wako ila ningeomba kufahamu zaidijuu ya mmiliki wa ile filamu ya girlfriend,mbona ukimsoma Shigongo naye hudai ni ya kwake?na ni kwa nini ulihama globalpublishers?

  10. Comment by FAD FADIA on March 29th, 2010 4:55 am

    Kk TAMBA kwnz hongera kwa kazi zako nzr na saport ulioitoa kwa wasanii wa filamu hapa nchini…Mungu akubariki sana…nilikuwa naomba mng kila cku anikutanishe na ww ili nipate mawazo yako,kifupi mm ni film & script writer na pia ni Director wa filamu mpya ya AMBISION na m2nzi wa LAST PROMISE ambazo zote zinakaribia kuingia sokoni,nina filamu nyng zilizokamilika zote ni prt 1 $ 2 zenye script zaidi ya 50 lkn cjajua niazie wp au nizifanyie nn naomba msaada wako/mfadfadia@yahoo.com/0653011313

Leave a Reply