MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

Ni vigumu sana kuzungumzia mashindano ya urembo nchini Tanzania hususani yale ya Miss Tanzania bila kumtaja Hashim Lundenga au Uncle Hashim kama ambavyo wengi hupenda kumuita. Sio tu kwamba Hashim Lundenga ndio aliyafufua tena mashindano ya urembo mwaka 1994 bali kampuni yake ya Lino International Agency Limited ndio haswa mratibu wa mashindano hayo ambayo kila mwaka yanazidi kuwa maarufu na hivyo kuwa tukio linalosubiriwa kila mwaka kwa hamu.

Kwa mwaka huu wa 2007,mashindano ya Miss Tanzania huenda yakawa yameandika historia mpya kabisa nchini Tanzania. Mshindi wa mwaka huu,Richa Adhia, ni mtanzania wa kwanza mwenye asili ya Asia (India) kutwaa taji hilo.Isitoshe ushindi wake umepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa watanzania jambo ambalo limebakia kuwa gumzo mpaka hivi leo.

 

Sasa ili kujua kwa undani kuhusu mashindano haya ya urembo huna budi kumuuliza Hashim Lundenga.Hivyo ndivyo tulivyofanya hivi karibuni katika mahojiano naye ambapo aliweka wazi nini kilimsukuma kufufua mashindano haya, anasemaje kuhusu ushindi wa Richa Adhia na nini watanzania tutegemee kutoka katika mashindano ya dunia (Miss World) mwaka huu? Pia Hashim anajibu swali ambalo limekuwa likiulizwa sana na wananchi;Je mashindano ya urembo ni kwa watoto wa “vizito’ peke yao?Haya hapa mahojiano kamili;

BC: Ulianza lini rasmi kujishughulisha na mashindano ya urembo? Ilikuwaje?

HL: Baada ya serikali kuamuru kufutwa kwa mashindano ya urembo mwishoni mwa miaka ya 1968 / 69 hapakuwepo na shughuli zozote za urembo hadi mwaka 1994.

Wazo la kurudisha upya mashindano ya urembo lilinijia baada ya mrembo wa kitanzania aitwaye Miriam Ikoa kushinda taji la urembo nchini Kenya. Kwangu niliona ni changamoto kwa vile niliona ni fedheha msichana wa kitanzania kufanya vizuri ugenini.

Nikaamua kuanzisha upya mashindano ya urembo nchini baada ya kufuata taratibu zote ambazo zilikuwa zinatolewa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Utamaduni [wakati huo] na chini ya Baraza la Sanaa la Taifa [BASATA] nikasajiliwa rasmi mwaka 1994 nikishirikiana na bwana Prashant Patel mfanya biashara ambaye alikuwa anamiliki hotel ya White Sands iliyopo Kunduchi jijini D’salaam. Toka mwaka huo mashindano yamekuwa yanakua mwaka hadi mwaka.

 

BC: Kumekuwepo na tafsiri mbalimbali kuhusiana na dhana “urembo”.Kwa mtazamo wako nini maana hasa ya urembo?

HL: Urembo ni sanaa. Urembo ni umaridadi, urembo ni hali ya mtu kujiremba kuwa msafi na kujiweka katika hali ya kupendeza.“Urembo sio uzuri” kuna wazuri na pia kuna warembo.

BC: Majuzi tulipoandika kidogo kuhusiana na mashindano ya mwaka huu ya Miss Tanzania mmoja wa wasomaji wetu aliacha swali akiuliza Tanzania imepata faida au hasara gani kutokana na mashindano ya urembo tangu mwaka 1994 mpaka leo?

HL: Tanzania inapata faida kubwa sana kupitia sanaa hii ya urembo kwa mfano:-

(1) Ajira: Mashindano haya yanasaidia sana kutoa ajira kwa washiriki na hivyo kuipunguzia mzigo serikali kwa kuwa na watu wengi wasio na ajira. Mchakato wa kumtafuta Miss Tanzania hufanyika nchi nzima. Kwa mkoa wa Dar-es-salaam kuna Vitongoji zaidi ya 15, Wilaya 16 kwa nchi nzima, na mikoa yote 20 Tanzania bara. Kuna Kanda 9 kwa nchi nzima na hatimaye washindi wa ngazi hiyo hushiriki katika fainali za taifa kila mwaka.

(2) Mashindano yote hayo hutoa ajira hata kama ni ya muda kwa makundi mengi ya jamii, kama mafundi cherehani, [kwa kushona mavazi mbalimbali ya warembo] mafundi seremala, [kwa kutengeza majukwaa [stage] n.k wapambaji, Washereheshaji, [MC] Wana muziki, wasanii wa kuchora, Matangazo, katika vyombo vya habari, na kadhalika, na kadhalika.

BC: Kwa muda sasa kumekuwepo na malalamiko kwamba mashindano ya urembo yanamdhalilisha mwanamke. Vazi la kuogelea ndio limekuwa likizungumziwa zaidi. Kwa mtizamo wako, kuna uhusiano gani kati ya udhalilishaji wa wanawake na mashindano ya urembo? Kama haupo unadhani malalamiko haya yanatoka wapi na yanatokana na nini?

HL: Ni lazima kwanza ufahamu kuwa mashindano yetu yanafuata taratibu na kanuni za mashindano ya urembo ya dunia, [Miss World] vazi la kuogelea likiwa ni sharti mojawapo, lakini ni vazi ambalo halitakiwi kumdhalilisha mtazamaji wala mvaaji mwenyewe. Miaka ya mwanzoni tulipata tabu sana na wanaharakati, lakini tuliwaachia wananchi wenyewe waamue, na walio wengi waliunga mkono vazi hilo liwepo. Katika vazi la ufukweni ndipo tunapo muangalia mshiriki / mrembo kwa vizuri zaidi umbo lake, kwani moja ya sifa ya ushindi ni lazima mshiriki / mrembo awe na umbo zuri. Sasa iwapo mshiriki / mrembo akivaa suruali au ushungi, utamuonaje umbo lake zuri?!??!Malalamiko zaidi yanatoka kwa wanaharakati nadhani unanielewa nikisema hivyo.

BC: Kumekuwepo shutuma kwamba mashindano ya urembo yanawabagua watu masikini kwani ili kuingia mashindanoni ni lazima ukawa na pesa kiasi fulani kwa ajili ya kununua mavazi,viatu nk. Unasemaje kuhusu hilo? Na je kama kuna ukweli ndani ya shutuma hizo ninyi kama kamati ya Miss Tanzania mnalishughulikiaje suala hili ili kuhakikisha hamkosi mrembo halisi kutokana na masuala ya kiuchumi?

HL: Mashindano yetu hayana ubaguzi kati ya watu masikini na matajiri, wote wanakaribishwa. Ni lazima ufahamu kwamba sanaa hii ya urembo inahitaji gharama kidogo, kwa mavazi, pamoja na kuhudumia mwili au ngozi ya mshiriki / mrembo. Ni lazima mshiriki / mrembo ajigharamie ili aweze kuonekana mrembo. Hatujawahi kupata malalamiko yoyote kutoka kwa mshiriki kwamba eti ameshindwa kwa sababu amekosa pesa za kujiremba na kuonekana mrembo, yapo mashirika hata watu binafsi ambao wapo tayari kumgharamia mshiriki kwa maana ya kumpa ufadhili / udhamini ili ndoto yake iweze kutimia.

 

Hashim Lundenga (katikati) akiwa na mbunge wa Kinondoni Idd Azan(kushoto) na katibu wa Baraza La Sanaa la Taifa Chief Shogholo Chali(kulia)

BC: Je ni kweli kwamba mojawapo ya vigezo mnavyovitumia katika kumtafuta mrembo wa ni wembamba? Kama ndio unadhani hii inapeleka ujumbe gani kwa watoto wadogo au watu wanene?

HL: Sio kweli kwamba mshiriki yoyote wa shindano la urembo ni lazima awe mwembamba, hata katika Taratibu na Kanuni za mashindano ya urembo ya dunia hilo halipo. Isipokuwa Majaji huamua kwa kufuata vigezo ambavyo kimoja wapo ni lazima mshiriki / mrembo awe na umbo zuri, sura nzuri, Tabasamu zuri, Haiba, Mcheshi, na Mwenye mvuto…washiriki wote wanakaribishwa wawe wanene au wembamba.

BC: Tangu Richa Adhia alipotangazwa kuwa mshindi wa Miss Tanzania 2007 kumekuwepo malumbano kadhaa juu ya ushindi wake. Katika mahojiano mengi ambayo umeshafanya na vyombo vya habari umeweka mambo sawa. Lakini ukweli unabakia kwamba kuna sumu fulani hivi ya ubaguzi. Je ninyi kama kamati ya Miss Tanzania, mna mipango gani ya siku za mbeleni kuhusiana na masuala kama haya ya “ubaguzi”?

HL: Kama nilivyokueleza hapo awali kuwa mashindano yetu hayabagui mshiriki yoyote yule anakaribishwa kwa kufuatana na vigezo, Taratibu, na Kanuni tulizojiwekea ambazo pia zimesajiriwa Serikalini kupitia Baraza la Sanaa la Taifa. Sifa za mshiriki ni kama ifuatavyo:

(1) Awe Raia wa Tanzania, raia anaweza kuwa kwa kuzaliwa, au kuukana uraia wake kama yeye ni raia wa nchi nyingine. Kwa maana hiyo kama ni raia kwa kuandikishwa basi atakuwa na Hati ya kuandikishwa uraia.

(2) Awe msichana wa miaka 18 hadi 23

(3) Awe hajaolewa wala kuzaa mtoto.

(4) Asiwe mwanafunzi wa shule ya msingi au Sekondari. [wanafunzi wa vyuo wanaruhusiwa]

(5) Mshiriki hatakiwi kushiriki zaidi ya mara 2 katika muhula mmoja, [yaani mwaka 1] huko nyuma kulikuwa na mtindo fulani, mshiriki hakishindwa kitongoji kimoja alikuwa anakimbilia kitongoji kingine. Hiyo hairuhusiwi.

(6) Mikakati tuliyonayo sasa na hapo baadaye ni kuelimisha umma wa Tanzania kwamba mashindano yetu hayana ubaguzi, na pia wananchi ni muhimu waelewe kwamba, nchi yetu inao raia wa rangi mbalimbali waliozaliwa hapa na wapo waliomba uraia kupitia Taratibu, Kanuni na Sheria zilizowekwa.

BC: Sasa kwa sababu mwaka huu Miss Tanzania ni “tofauti” na wa miaka iliyopita, watanzania tutarajie nini? Ushindi?

HL: Ushindi ni muhimu lakini hatuwezi ku-guarantee ushindi hivi hivi tu, , kwa sababu kila palipo na mashindano kuna washindi na watakaoshindwa, Miss Tanzania tayari tumeshaingia fainali za dunia za mashindano ya urembo mwaka 2005 kwa mrembo wetu Nancy Sumari kutwaa taji la Miss world Africa na kuwa miongoni mwa warembo 6 bora wa dunia [TOP6 FINALIST]

Tunacho kitafuta sasa ni ushindi wa dunia, yaani Miss world title. Hatuwezi kujua, lolote linaweza kutokea, kwani hata kwa mrembo Nancy Sumari kuna baadhi ya wadau walibeza ushindi wake hapa nchini na baadaye tulipoibuka kidedea wakabaki wakishangilia. Lolote linaweza kutokea.

BC: Kama kamati ya Miss Tanzania mnamuandaaje mrembo wetu wa mwaka huu kabla hajaelekea China? Mnazingatia mambo gani? Nini majukumu yenu katika maandalizi yake?

HL: Kamati inazingatia zaidi Kanuni na Taratibu za mashindano ya urembo ya dunia, mrembo wetu kwa sasa yupo katika hatua za mwisho za maandalizi kwa maana ya mavazi, na mafunzo mbalimbali ya nadharia na vitendo, yahusuyo mashindano ya urembo. Jukumu letu ni kuhakikisha kila nyanja muhimu tuna mhudumia kuanzia Usafiri, Mavazi, na mahitaji yote ya kisaikolojia…

BC: Zaidi ya masuala ya kuratibu mashindano ya Miss Tanzania, kampuni yako ya Lino inajishughulisha na nini kingine?

HL: Kampuni ya Lino International Agency Limited, ni kampuni inayohusika zaidi na masuala ya burudani, Entertainment, Event management, Sports activities, Public Relations, Consultants, pamoja na shughuli zingine za clearing and forwarding.

BC: Unalo lolote ambalo ungependa kuongezea kuhusiana na mashindano ya mwaka huu?

HL: Mashindano ya mwaka huu 2007 yalikuwa mazuri tu na tofauti kidogo na ya miaka ya nyuma. Tofauti yake ni kwamba yamefanyika katika eneo la wazi, open space, jukwaa pia lilikuwa zuri na tofauti na miaka ya nyuma, hata upande wa burudani pia ulikuwa tofauti. Hii ndio JIONEE TOFAUTI na Vodacom na mrembo aliyeshinda pia ameonekana tofauti kiasi cha wadau kuanza kupiga kelele.

Nawasihi tunyamaze, tumpe ushirikiano, tumuombee duah kwa Mungu, ashinde katika mashindano ya dunia, kwani ushindi wake si wa kwake pekee yake bali ni wa taifa la wa – Tanzania wote…Asanteni sana.

PICHA ZOTE KWA NIABA YA MICHUZI JR.

Share and Enjoy:
  • Digg
  • Sphinn
  • del.icio.us
  • Facebook
  • Mixx
  • Google Bookmarks
  • email
  • LinkedIn
  • Live
  • Spurl
  • Technorati
  • Yahoo! Buzz
  • YahooMyWeb

Feedback / Comments

45 Responses to ““UREMBO SIO UZURI”-HASHIM LUNDENGA”

  1. Comment by Dinah on September 26th, 2007 11:48 am

    Nimeguswa kidogo kwenye swala la mrembo kujigharamia kwenye mavazi, utunzajiwa ngozi ambo hakika ni mgumu ikiwa ulikuwa huijali ngozi yako hapo awali.

    Washiriki wengi wanaojitokeza kwenye haya mashindando wengi wako shule ama ndio wamemaliza masomo wanasubiri majibu kwenda Uni. Ni wazi kuwa hawana kipato cha kutosha kugharamia yote hayo.

    Kwa mwanajamii wa kawaida ataona wazi (well mimi ndio nadhani hivyo) kuwa hilo litamsukuma binti kufanya ngono holela au kufanya tendo hilo na yeyote atakae offer bulingutu au udhamini ili kujikimu na kuwa mrembo ili ashiriki mashindano ya Urembo na hatimae Miss Tz.

    Lundenga kama mzazi, mjomba, mlezi na mume huoni kuwa kampuni yako na zile zinazosimamia mashindano ya urembo ya awali kuwadhamini washiriki hao wadogo kwa maswala ya mavazi na urembo kwa ujumla(ulaji, utunzajiwa ngozi n.k.)?

    Mahojiano mazuri ila Lundenga majibu yako yamekaa kimimi-mimi yaani kibinafsi.

    Big up to BC, kazi munono!

  2. Comment by Dinah on September 26th, 2007 11:56 am

    oh nilisahau, kwanini kila Mshindi wa Miss Tz lazima atoke Dar? Ukiacha yule mmoja alitoka Morogoro well nafikiri aliwakilisha mkoa wa Moro lakini makazi yake ni dar.

    Lingine ni hili kwanini washiriki wengi ambao wanaishi Dar wanakimbilia Mikoani kugombea Miss Mkoa husika hali wakijua kuwa si wakazi wa huko?

    Ktk hali halisi ni kuwa walioishi Dar hujiona wajanja zaidi na kujiamini sana zaidi ya wale waishio mkoani hapo.

    Hamuoni huko ni kuwanyima nafasi washiriki ambao ni wakazi wa mkoa husika ili kuwapa challenge na hivyo huenda siku moja tukatoa Binti bomba wa kuwakilisha Bongo?

    Mnaonaje mkiongeza kipengere cha kuonyesha tamaduni ya mshiriki( kucheza ngoma au vazi) kutoka mkoa husika ili kuongeza burudani na kukumbusha watu kuwa hey pamoja na maendeleo bin uigaji tunajali nakutukuza tamaduni zetu.

    Najua Lunde Utasoma hii.

    BC mtafuteni Q-Chillah basiii!

  3. Comment by mesa on September 26th, 2007 1:03 pm

    urembo ni kugawa mpenyo ili ushinde mweeeeeeee

  4. Comment by nefertiti on September 26th, 2007 1:33 pm

    Dada Dinah napenda maelezo yako na ninaafiki kabisa… nataka kuongezea tu kuwa ni waTanzania kama akina Lundenga wenye uchu wa maisha (high life style) nakuweza kuuza utu wao bila kufikiri.

    Lundenga kaanzisha huu mradi siyo kwa sababu ya Uzalendo bali kwa ajili ya kupenda Ngono (najaribu kutumia maneno ya kiustaarabu kidogo….. kwa hiyo kajipatia kihalali ukumbi wa kuendeleza hayo.

    Wakina HL wanajifanya kuwa wanamaendeleo kwa kuiga tamaduni za kigeni bila tathmini ya kuona inaathiri vipi jamii waliyozaliwa (kwa bahati mbaya).

    Hana jibu la maana juu ya mtoto wa kihindi kushinda huo Umiss TZ kwa sababu yuko mifukoni mwa mabwana (wahindi).

  5. Comment by nefertiti on September 26th, 2007 1:39 pm

    Namkumbusha tu Hashim kuwa kwa Dini na Utamaduni wa Mtanzania katuuza wazawa wa nchi hii – akina Kidawa na Sekibabala – kama ni usanii (Art) kweli basi nayeye anao mabinti basi naAwaanike kwenye Ulimbwende huo – mwezi wa Ramadhani mzima haogopi kuwa kuna kufa na kiyama. TAFAKARI HASHIM LUNDENGA>

  6. Comment by Moses Jakanyangoe on September 26th, 2007 2:04 pm

    Kama kweli nchi iko makini inafaa haya mashindano yawe katika miliki ya serikali na siyo kampuni binafsi!…Kama serikali haiwezi kuyasimamia, basi itolewe tenda ya wazi na makampuni kadhaa ya nchini hata kutoka nje yapewe kazi ya kuratibu na kusimamia mashindano haya. Kama kila mwaka ni hawa akina Lundenga na jamaa zake tu ambao upeo wao ni mfupi bado kutakuwa na malalamiko tu. Hata hivyo hii miaka 13 tangu yaanze upya sioni kama tuna la kujivunia kwenye fani hii!

  7. Comment by Dinah on September 26th, 2007 2:37 pm

    Nakubaliana na Moses.

    Nimetafakari majibu yake nikagundua huyu jamaa hajabadilika/kua kiakili.

    Kaulizwa Tanzania imefaidika nini? Kajibu (nanukuu) “Ajira: Mashindano haya yanasaidia sana kutoa ajira kwa washiriki na hivyo kuipunguzia mzigo serikali kwa kuwa na watu wengi wasio na ajira.

    Mchakato wa kumtafuta Miss Tanzania hufanyika nchi nzima. Kwa mkoa wa Dar-es-salaam kuna Vitongoji zaidi ya 15, Wilaya 16 kwa nchi nzima, na mikoa yote 20 Tanzania bara. Kuna Kanda 9 kwa nchi nzima na hatimaye washindi wa ngazi hiyo hushiriki katika fainali za taifa kila mwaka.”

    Jamani washiriki wa mashindano hayo hawafikii idadi ya shule moja ya msingi hapo Dar sasa utasemaje kuwa Serikali inapunguziwa mzgo kw avile washiriki wanapata ajilira via mashindano hayo?

    Nadhani angesema kuwa inawasaidia washiriki kupata ajira kwa urahisi kutokana na urembo wao au kile kitendo cha kushiriki “miss Tz” na sio Tz kama nchi.

    Kampuni inajishughulisha na mambo mengi ikiwa ni pamoja na “Public Relations”, ikiwa wewe hujui kujieleza na kujibu maswali vema nina wasiwasi na huduma ya U-PR.

  8. Comment by Mgumu on September 26th, 2007 2:49 pm

    Kwa kweli mimi nakubaliana na Dina pamija Nerfertiti na Moses, Kwakweli mmeandika vizuri sana. Natamani nyinyi ndio mngekuwa majaji.Mr Lundenga hajui alisemalo na kama Dina alivyosema yamekaa kimimimiCha muhimu ndugu zangu iliyobaki apewe madaraka mtu mwingine au serikali iweze kusimamia kwani tuna mawaziri wengi mfano kuna waziri wa michezo kwanini nae hasisaidie ktk mambo ya Umiss.
    Shukrani kwa wote

  9. Comment by Lizzie on September 26th, 2007 3:12 pm

    Mimi nashindwa hata niweke vipi maana hata serikali ukiwapa ndio kwanza itakuwa ulafi wao,ukisema watangaze tender every season watataka kuongwa na wampe tender mtu asiye na viwango basi mimi nimejichokea ngoja ni nyamaze tu wote hata juu mmeandika vizuri sana

  10. Comment by muddy on September 26th, 2007 3:45 pm

    Hata hivyo imetosha wewe na timu yako kuandaa mashindano hayo msiwe ving’ang’anizi kama kamati ya olimpiki ya miaka ileeeeeee ya kina rafael kubaga – WAACHIENI WENGINE!!!

  11. Comment by Kenny on September 26th, 2007 4:01 pm

    Kwa kweli interview ni nzuri, maswali mliyoyauliza ni muhimu sana, lakini nakubaliana na wenzangu hapo juu, Dina na Moses, kwa kweli Hashim ametuangusha na majibu aliyoyatoa. Inasikitisha hata yeye anakubali mwenye pesa ndio anaeweza kushindana katika u Miss Tanzania, kwanini basi wasiite jina lengine, kwani watanzani sio wote wenye uwezo huo unaombatanisha na mashindano. Ukiangalia sana ndio maana hata washiriki wengine unajiuliza wamefikaje pale, kama tunatafuta mtu mwenye uwezo wa kutunza ngozi, then hatutafuti natural beauty. Mimi naona inabidi wazingatie natural beauty kwanza, hivyo itaweza kuwahusisha wasichana walio wazuri. na kama wengine walivyosema inabidi serikali ijaribu kufanya usawa, iwape watu tofauti tofauti katika hii kazi, Lazima tuelewe kuwa huyu Miss Tanzania anaenda kupresent Tanzania. kuwe na usawa kwa watanzania wote kushiriki na ku run hiyo process nzima. OOh alafu kumbe partner wa huyu jamaa ni kina Richa!!!Haya tuone mbele…

  12. Comment by Bob Sankofa on September 26th, 2007 4:12 pm

    Nafikiri Lundenga ana falsafa sawa kabisa, urembo si uzuri. Inabaki hivyo.

    Lakini naomba nitofautiane kidogo na uncle Lunde kwa kudai kuwa hata “wanene” wanakaribishwa kwenye mashindano yale ya urembo. Kama anavyosema kuwa mashindano yale yanafuata viwango vya Miss World, ambayo ni ya wazungu zaidi, kwa kweli wanene hapo hawana nafasi kabisa, wakituvalia vinguo vya ufukwe patakuwa hapatoshi ukumbini. Tuache tu “wembamba” waendelee.

    Napenda kuipongeza kampuni ya Lino kwa kuwezesha kufanyika mashindano ya urembo kwa muda wa miaka kumi na tatu bila kigugumizi. Tunayafahamu makampuni kibao ambayo yaliwahi kuandaa mashindano ya vitongoji na wakalala mbele na zawadi, wasiweze hata kuandaa mashindano ya mwaka uliofuata. Hongera Lino.

    Kuhusu, Richa nimeshasema vya kutosha, naomba nisiseme tena hapa kwani si mahala swadakta kwa sana.

    UHURU!

  13. Comment by Tack on September 26th, 2007 5:00 pm

    Mr Lundenga ananimaliza anavyosema Miss hatakiwi kushiliki mara mbili kwenye vitongoji, tukiacha vitongoji mbona Richa alishakuwa miss Utalii? Au kwasababu vitongoji haviingiliani na utalii? Pia sheria ya MISSWORLD inasema wanataka miss ambaye kashiriki mara moja tu.Sasa mbona Lundenga anampeleka mtu alishashindwa huko China na bado anampeleka tena
    Kwa kweli nashindwa kumuelewa ni ngumu sana.

  14. Comment by Miu on September 26th, 2007 5:22 pm

    Jamani hata wanene? basi inabidi tujiandae wengine
    Manake Bosi Lundenga kashasema.

  15. Comment by Isaac on September 26th, 2007 8:06 pm

    Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Bw. Hashim Lundenga na washirika wenzake kwa kuweza kufufua na kuyaendesha mashindano ya Miss Tanzania kila mwaka na mafanikio ambayo yamekwishapatikana.
    Ukweli ni kwamba ni wachache miongoni mwetu ambao tunajua na kufuatilia sheria na taratibu zinazohusiana na mashindano haya, wengi wamekuwa hata uchangiaji wao unaonyesha mapungufu katika kujieleza na kutambua ni nini kina husiana na masula ya urembo.
    Ningependa kutoa ushauri kwamba (kama itawezekana) kamati ya miss Tanzania iendeshe semina maalum kwa waandishi wa habari za urembo ili waweze kuandika sawia yahusuyo Miss Tanzania na urembo kwa ujumla. Japokuwa nina wasiwasi kama watanzania walengwa watasoma, kwani hatuna utamaduni wa kujisomea hasa ifikapo kujisomea kwa kupata maarifa.
    Sina haja ya kurudia alichoandika Bob Sankofa hapo juu, lakini kuendesha mashindano kama haya bila ya kigugumizi kwa muda wote huo, na huku kamati ikikabilwa na changamoto mbalimbali yakukuza fani hiyo, kwa kweli sijambo la kubeza hata kidogo, ni kazi kubwa sana na wakati mwingine unaweza kutatamaa kama huna moyo na nia thabiti.
    Tusiache kuwakosoa kwa maana ya kujenga kwani wao sio malaika hawawezi kuwa right all the time.
    Namalizia kwa kuwatakia mafanikio zaidi na zaidi

  16. Comment by Mwasi on September 26th, 2007 9:00 pm

    Mimi naona kamati ya maamdalizi ya urembo ibadilishwe, thats all.

  17. Comment by Pope Pius on September 26th, 2007 11:01 pm

    Inashangaza maana majaji huwa wanakuwa na majibu kabla kwani Pre-Judgement huwa inafanyika siku kadhaa kabla hapo inakuwa vigumu kwa mrembo hata akijitahidi kwa siku zilizobaki afanye vizuri, nafikiri wazo ni zuri la mashindano, ila mfumo unafaa kurekebishwa
    1. Unawapa upendeleo zaidi washiriki wa Dar kwani inakuwa kanda nyingi, vitongoji vingi na hatimaye kila wilaya kuingia kama mkoa, hii haiwapi fursa sawa washiriki wa mikoani kwani hata huko wawakilishi ni watoto wa Dsm ambao hukimbilia mikoa dhaifu ili washiriki kama walivyotangulia kusema wenzangu.

    2. Hashim anashindwa kuwafanya watu waelewe hasa kigezo cha kumpata mshindi au muwakilishi, namaanisha hawezi kujieleza kutokana na maswali kwani maswali aliyoulizwa ni mazuri ambayo yalitaka majibu makini ila anakurupuka tuuu kaaa Juha!!

    3. amesema kamati inazingatia kanuni na muongozo wa mashindano ya dunia sasa mbona anasema wanene wanakaribishwa?

    4. Nafikiri ni wakati muafaka mashindano haya yakaratibiwa na Wizaraya ya Michezo au Utamaduni then itoe Tender kwa Kampuni husika ili walao ushindani na nia madhubuti iwepo kwa waandaaji kwa mtazamo wa Interest ya Utaifa zaidi na si mfuko binafsi.

    kwa sasa ni hayo tuu Uncle Hashim.

  18. Comment by Nas on September 27th, 2007 12:41 am

    WATANZANIA WAMEUZWA THIS TIME NI AIBU SANA. KILA MTU HUKO CHINA ATAENDA KUWAKILISHA UTAMADUNI WA NCHI YAKE HUYO RICHA WENU ATAWAKILISHA UTAMADUNI GANI WAKATI HATA KISWAHILI HAJUI??? HASHIMU ROHO HAIKUSUTI? UZALENDO WA NCHI YETU UKO WAPI?? TUTAJIUZA HIVI MPAKA LINI JAMANI?? ROHO INAUMA SANA!!!!

  19. Comment by stambuli on September 27th, 2007 1:33 am

    Ukweli ambao watu wengi hawataki kuukubali ni kwamba haya mashindano yanawadhalilisha Dada zetu kwa kuiga tamaduni za kizungu,Hivi ni nani mwenye akili zake Timamu anaweza kukubali Dada yake aonyeshe mwili wake ili apate Zawadi,Huku ni sawa na kujiuza na ndio maana wanajaribu kuweka zawadi nyingi nzuri ili kuwavutia watu wakae Uchi na wanaopenda kuangalia watu wanaokaa uchi Hushangilia kwa kisingizo cha Urembo.Waondoe Zawadi kwa warembo kama watapata mtu atakayekubali kujidhalilisha mbele ya kadamnasi.Huu ni uchangu doa ambao unaratibiwa na makampuni yaliyosajiliwa na ndio maana tuhuma za vitendo vya ngono kwa dada zetu zimekuwa nyingi kwa sababu wanataka kuishi maisha ya Hali ya juu ambayo hayaendani na uwezo wao wa kiuchumi.Niliwahi kusikia mahaojiano ya Mustafa Songambele anaelezea wakati mashindano haya yanafanyika kwa mara ya kwanza yeye alikuwa Mkuu wa mkoa,baada ya yale mashindano asubuhi kutoka kwenye magazeti,aliitwa na Julius Ikulu.Alichoambiwa na Julius ni kwamba hataki kusikia uchafu ule na ndio ukawa mwanzo na mwisho wa mashindano ya urembo mpaka Julius kaondoka madarakani.B.C.imtafute Songambele an full story yupo Songea analima.Naona kuna hatari mashoga nao wakadai mashindano yao.Lundenga Muogope mungu wako halafu ukifa unataka watu wakuombee Dua kwa Mungu.Mungu gani wa Ulaya anayeruhusu watu wakae Uchi au Huyu Allah anayekataza Uchafu Huu.Huu ni Uchafu Ondoeni.
    By.Stambuli

  20. Comment by zoe on September 27th, 2007 2:58 am

    people!!!!acheni fikira potofu nyie binadamu. hivi mnafahamu ni mambo mangapi nyie mnaojiita watanzania mnafanya ambayo yote yapo kinyume na maadili ya kitanzania,mbona hamvai magome ya miti na kaniki kama mababu zetu walivyokuwa wanavaa??? au kuvaa nguo hamjui si tamaduni yetu?????? mbona mnaongea kingereza lugha ya watu,mbona mnatumia dining tables,mbona tunatumia tovuti kwa kuangalia pornogarphy, au yote hayo ni ya Utamaduni wetu?????
    Hebu kuweni watu wa kufikiri na mjue mambo ya kupotezea muda kwa argue,au mnafikiri Football,basketball,boxing hiyo yote ni michezo iliyotokana na utamaduini wetu????? Hata hizi blogu unafikiri ni utamaduni huuu,fungueni Macho nyie malimbukeni…..To cut the long story short ni kwamba ni kweli Miss Tanzania(Any Beauty Peagent) si utamaduni wa Mtanzani(Mwafrika) ila yote hayo tunaiga kutoka huko Ng’ambo. Kwahiyo nisingependa Miss Tanzania ipigiwe kelele peke yake,kwasababu tunaiga mengi lkn hamsemi ni hilo tu ndiyo mnafungulia mdomo.

  21. Comment by maya65 on September 27th, 2007 3:28 am

    huyu jamaa sijui lundenga au ludenga hatufai, afadhali hata wizara ya utamaduni na michezo ingesimamia haya mashindano ya umiss!!!!
    kila siku ni hao hao tumechoka tunataka mabadiliko…hawa jamaa akina lundenga naona wanadhalilisha utamaduni wetu na wewe jamaa hapo juu uliesema eti “kama tunajali utamaduni basi tuvae magome ya miti” naona una fikra finyu na pengine ulifeli somo la history !!!!!!
    we want changes now we dont need same faces everyday !!!!!

  22. Comment by Rose on September 27th, 2007 4:17 am

    LUNDENGA UMENIBOA SANA KUMPA MHINDI BENDERA YA TAIFA LETU. HIVI WEWE HAO KINA TANIL WAMEKUHONGA SANA EEH, MANAKE HAIWEZEKANI UMPE MHINDI BENDERA YETU LUNDENGA UMETUTIA AIBU YA KARNE. UMENIBOA SANA YAANI SITAMANI HATA KUKUONA. BORA UJIUZULU MANAKE WEWE UNAOPENDA SANA RUSHWA HASWA KWA WAHINDI AMBAO NDO WADHAMINI. KWELI TUMEISHIWA WAREMBO MPAKA TUNAWAKILISHWA MA MHINDI. BORA ANGEKUWA HANA PUA NDEFE, MANAKE NAONA HATA AKISHINDA ATAENDA INDIA HATOKUJA TZ. UMENIUDHI LUNDENGA, HUFAI KABISA WALLAHI!!

  23. Comment by Willy "the goal getter" on September 27th, 2007 8:13 am

    Lundenga ameuza taji kwa mabosi zake WADOSI kwa sababu ya offer anazopewa bila kusahau na lunch hapo kwa Dewji (hadees sijui) karibu na ofisi yake.
    Serikali iyabinafsishe hayo mashindano tuingie mkataba kama tunavyoingia mikataba mbalimbali kama vile ya b……….gi.

  24. Comment by Materego Jr. on September 27th, 2007 8:39 am

    KAMA ALIVYOSEMA KAKA YANGU WILL HAPO JUU WAKATI UMEFIKA SASA TENDA ZITANGAZWE ILI KUWAPA CHALLENGE HAWA AKINA LUNDENGA NA WAHINDI WAKE ILI WAJUE HAYA MASHINDANO SIO MALI YAO NI YA WATANZANIA WOTE PIA NAFIKIRI KUWE NA KANUNI ZILIZO WAZI KWA WAGOMBEA U MISS KUEPUKA UPANGAJI WA MATOKEO. KUSIWEPO NA HIYO PRE JUGEMENT YAO KWANI THROUGH IT NDIYO WANAPATA NAFASI YA KUWAPA TAJI WATU WAO NI HAYO TU KWA SASA.
    kAZI NZURI BC KEEP IT UP!

  25. Comment by Baraka on September 30th, 2007 7:18 am

    Moses na Dinah nyie ni waosha vinywa tu,

    Moses unasema miaka 13 imepita hakuna tuliloona la manufaa.

    NANCY SUMARI alitoka pia kwa Hashim Lundenga, lakini kama tunavyowajua watanzania kila wakati kulalamika tu, na sio kulalalimika tu nakusahau pia.

    Kuwapa challenge akina Lundenga kwamba mashindano sio mali yao tu bali ya watanzanani wote, ebo hata nyie kama mna nafasi yakuanzisha mashindano kama mnafuata sheria na kanuni za nchi mnaweza kuanza mashindano yenu.

    Na mwisho, huyo msambaa anayejiita Stambuli, siku hizi Bongo tuna uhuru au at least tunaweza kuchagua channel kwenye TV. kama ni siku ya mashindano na yanaonyeshwa kwenye TV basi badilisha channel ili usione hao unaosema wanatembea uchi.

    Mnaboa

  26. Comment by TanzanianDream on October 2nd, 2007 10:03 am

    Kusema ukweli hakuna mwelekeo kabisa kwenye Urembo…Richa alisema Ngorongoro ipo kwenye maajabu 8 ya dunia,Lundenga anasema Tanzania Bara ina mikoa 20 kweli hawa ni Watanzania au ndo tumekabidhi mikoba kwa Mgeni?Nway bado anajibu maswali kwa UTAJIJU nyingi anasahau huo Urembo sio wake ni wa WaTZ haya jamani wale wazungu wenye uraia wa Bongo nao wameruhusiwa mradi waoneshe Passport zao tu kweli kuna kazi….Pamoja.

  27. Comment by Ed (USA) on October 4th, 2007 4:23 am

    Sijui masuala ya urembo kwani sijajiingiza huko kwasababu zangu binafsi. Lakini kwa kutumia common sense baada ya kupitia mawazo humu ndani, haraka haraka naona analaumiwa bwana Lundenga kama vile amempa ushindi wa miss Tanzania mhindi. Maswali nauliza, hivi kwenye hayo mashindano Lundenga ndio alikuwa Jaji? Tanzania haina raia wahindi? Nchi nyingine duniani hazina raia waliotokea Tanzania?

    Japokuwa kibinadamu naelewa Lundenga atakuwa na makosa lakini si sawa kumbambikia makosa yasiyostahili. Kwa kuwakumbusha mliosahau historia ya bongo, viongozi waanzilishi huko nyuma hawakuwatimua wahindi katika nchi hii kama alivyofanya Idi Amin kule Uganda. Mashindano yoyote yanayosimamiwa na majaji, wakulaumiwa ni majaji iwapo kuna hitilafu imejitokeza. Watanzania tujifunze kushambulia wakosaji kwa vigezo na sio kutumia mbinu za wapiga ramli. Ukitembea duaniani nchi mbalimbali zina raia tofauti toka mataifa mbalimbali. Mimi nina mtoto mmarekani sasa akisakamwa huku kama huyo mhindi nitajisikiaje?

    Nijuavyo mimi kwa upeo mdogo nilionao, mambo mengi tunacopy toka kwa wenzetu waliotutangulia. Sasa inakuwa ni vigumu kuendana na tunavyotaka sisi kwasababu tunacopy mpaka kanuni zake pia ili kuleta msisimko sawa na original yake. Mfano mzuri ni mpira wa miguu. Tukisema turekebishe kanuni tuendeshe tunavyotaka sisi, tutakwama kwenda mbele kiafrica na kimataifa.

    Naomba tujifunze kutoa hoja za msingi tuache chuki hazitatufikisha popote.

  28. Comment by Malonga on October 4th, 2007 4:46 am

    Kwanza acheni huyu binti atuwakilishe kwa sababu zifuatazo – Katika mashindano yoyote Miriam Odemba hakuna mshiriki ambaye alijiwakilisha akiwa katika hali yake halisi kwani kila mchu alijiremba kuanzia ngozi hadi nywele kama Mhindi sasa kwanini asichukuliwe mhindi halisi kwani dada zetu wote wamekuwa wakiukana utanzania wao halisi acheni za kuleta. Huyo hada gharama yoyote na wala hakani asili yake halisi – Nadhani hilo litakuwa fundisho kwenu – Kiwakilisheni kwa kipilipili chenu na weusi wenu halisi kwanza kujibadilisha kwenu ndiko kunafanya tukose ushindi.

  29. Comment by Mnyandwa on October 4th, 2007 5:30 am

    Kwanza napenda kuwapeni pole wale wote ambao hawakuridhika na ushindi wa Richa Adhia. Hata mimi ni mmoja wao kwani iliniuma mnao lakini tufanyeje zaidi ya kufanya marekebisho zaidi mwakani?

    Ni muda mrefu tangu Bwana Lundenga aanzishe mashindano ya urembo na katika kipindi chote cha ufuatiliaji wangu ni mrembo mmoja tu ambaye hata akisimama kumpinga Richa nitamuunga mkono – waliobakia wote mpende msipende ushindi huu hamna budi kuunga mkono kwa sababu zifuatazo:-

    1) Wote wanazipenda na wamekuwa wakiwakilisha nywele
    za kihidi.

    2) Walembo wote wamekuwa hawapendi kujiwakilisha
    katika ngozi (rangi) zao halisi ila lazime
    ziwe kama za kihindi.

    3) Kila mara wamekuwa wakipendelea mavazi ya
    kihindi wakiacha vitovu nje vazi la baniani).

    Sasa iweje leo ashinde ambaye yuko katika hali yake halisi leo iwe nongwa?

    Jamani tusipoteze muda kwa malumbano acheni huyu binti atuwakilishe na asili yake ya kihindi kwa vigezo hivi kwanini asichukuliwe mhindi halisi kwani dada zetu wote wamekuwa wakiukana Utanzania wao halisi. Huyo hana gharama yoyote na wala hakani asili yake halisi. Hakuna sababu ya kumlaumu Lundenga wala majaji uhalisi nao ni kigezo tosha – Nadhani hilo litakuwa fundisho kwenu – Jiwakilisheni kwa kipilipili chenu na weusi wenu halisi kwanza kujibadilisha kwenu ndiko kunafanya tukose ushindi.

    Hili mwaliona ni dogo ni kubwa kwa kimataifa pia.
    Hatuna budi kumtakiya safari njema Richa – Kaza buti mwanangu. Tuletee taji ili uweze kujisafisha.

  30. Comment by Nana on October 4th, 2007 2:05 pm

    Mheshimiwa ED U S A Umesema mtoto wako ni half U S na TZ yeye kashakuwa na damu yako.Mbona tulikuwa na Miss jina lake Angel Damasi yeye mwenyewe ana damu nyeusi na ya kizungu na alishinda na watu tulimkubali, kutokana na damu yake, Sasa yule MISSINDIATZ ni pure india anadamu ya mtu mweusi.Sasa jamii ya watanzania haitomkubali yeye ni mwindi tu.Kwanza alishakuwa miss utalii na hakashindwa na bado wa kampa huyohuyo miss Tz.Wewe mwenyewe binafsi huoni kama kuna kitu kimefanyika paka yule kashinda Miss Tz.WATANZANIA TUHAMKE NDUGU ZANGU

  31. Comment by Nana on October 4th, 2007 2:35 pm

    Kwa kumalizia kusema waliodhamini hayo mashindano ni Waindi na Mpambe wao Lundenga na voda. Mbona kulikuwa na wasichana wazuri kutoka mikoani na walikuwa hawana nywele za bandia na wako natural(BLACK BEAUT)na walivaa vizuri mavazi yao ya kawaida.Lakini kutokana na Bongo kujuana na kuonga matokeo yake ndio hayo.NADHANI HAYA MASHINDANO YAME KAHAA KIMIPANGOPANGO

  32. Comment by Ed (USA) on October 5th, 2007 3:38 am

    Mheshimiwa Nana, kama nilivyosema sijajiingiza kwenye fani hii kiasi kuweza kujua mengi. Hivi kanuni zinazotumika zinataka mtanzania damu kama unavyosema au raia? Kama kigezo kipo kwenye uraia na huyo mhindi ni raia basi anasifa kushindana. Ingekuwa vizuri hapa lawama zipelekwe kwa majaji na kama Lundenga alikuwa jaji basi ni kawaida kwa mashindano yoyote kutokea malalamiko. Na kama tunakubaliana alistahili kushindana, mimi sidhani kama alikosa chance ya kushinda kutokana na vigezo vilivyowekwa. Na kama una uhakika wa kuhonga au kupendelewa kwa shinikizo la waandaaji, ni vizuri ukatoa uthibitisho na sio kuhisia tu.

    Kwa hii point yako ya Utanzania damu. Ikiwa ameshiriki mpemba yule mwenye damu ya mwarabu pure hapo utasemaje? Kama haufahamu wapo warabu, wachina n.k. ninaowafahamu mimi wamezaliwa na kukulia bongo na hata huko kwao hawakufahamu. Sasa hawa tutawaweka katika fungu lipi katika point yako ya Tanzania damu damu?

    Hapa katika mjadala huu tunakosa kuelewa nini madhara ya ubaguzi wa rangi na umuhimu wa kujua elimu ya uraia. Mimi sina ajenda yoyote ya kumtetea miss Tanzania kwanza namuona kwenye picha tu nikiwa huku mbali na nyumbani. Ninachokereketwa kuandika tena kwa mara nyingine, ni kushauri tutoe point za msingi tukiweka chuki pembeni. Tukosoe kwa hoja za msingi sio kupayuka kwani wengi wataelimika kwa kusoma hoja za maana na sio bla bla.

  33. Comment by TanzanianDream on October 5th, 2007 8:15 am

    Wow Ed,kweli unatumia akili/elimu au unatumia nini?Mi nna nia ya kukupinga siwezi kuwa mnafki…Umetoa mfano mzuri wa waarab tuache wapemba(unguja,pemba,mafia n.k) ambao hawashiriki kutokana na mila na desturi za eneo lao.
    Binafsi huyu dada uhindi wake ni kikwazo lkn pia uzuri wake ni tatizo…Wanaowajua wahindi kuna dada(mdada) anaitwa Aishwarya Rai alishinda Miss World 1999 if not mistaken kama yule ndo angeshinda bongo watu sidhani kama wangehoji sana ila huyu Richa wa kawaida mno kusema ni xtraordinary kwa opponents wake….

    Angeshinda muarab siamini kama watu wangejitokeza wengi kiasi hiki kumpinga kutokana na sababu zifuatazo:
    1.Wapo waarabu wabaguzi lakini wengi sio wabaguzi na tuliokulia uswahili tutakuwa tumeona mifano wanavyojichanganya.

    2.Muarab haishi kwa kujitenga,nenda Kisiju,Tandale,Masaki,Stesheni kote utamkuta.

    3.Na kubwa kuliko yote ni historia Muarab alitawala eneo la Tanganyika na znz kwa maana hiyo historia yake inamlinda zaidi.

    Lakini huyo mhindi unayemtetea wewe japo hutaki kuweka bayana ni wazi ni mfano wa ubaguzi uliopo Tanzania…Bado Lawama zinaenda kwa Lundenga maana wao ndo wanaopokea fomu za kujiandikisha huo umiss kwahiyo kwa njia yeyote yeye na kampuni yake ndo walengwa namba moja…Sidhani kama huyo gabachori(kwa lugha ya kibaguzi kabisa)kama angekatazwa kuchukua au kurudisha fomu yake tungekuwa tunaongea haya….

    Mwisho point ambayo wengi wameiongelea ni kuwa huyo Binti alishiriki mwaka jana kwenye mashindano ambayo hayana msisimko kama Miss World akashindwa je kwenye mashindano ambayo vigezo vyake ni vikubwa na imara zaidi atawezaje kushinda….

    Ubaguzi upo na mimi nipo kwa wahindi wenyewe kwahiyo naongea with more Xperience zaidi yako maana huwajui hawa watu KWA MANENO MACHACHE NI WABAGUZI SANA TENA SANA….

    Mwisho hakuna mtanzania ambae analalamika bure hapa ila kutokana na uchungu alionae kwa wahindi,tumeona na kuishi ubaguzi wao kwahiyo kila mtu anaongea kwa uchungu na nchi yake,msalimie mwanao.

  34. Comment by Nana on October 5th, 2007 12:37 pm

    Asante TANZANIADREAM KWA KUNIELEWA VIZURI MUNGU HAZIDI KUKUPA.

  35. Comment by Ed (USA) on October 6th, 2007 1:51 pm

    AFADHALI NDUGU YANGU T.DREAM UMEWEKA WAZI KUWA TUNA TATIZO NA WAHINDI HUKO NYUMBANI KUWA NI WA WABAGUZI NA WANAJITENGA. KUMBE MALUMBANO YOTE HAYA MZIZI WA FITINA HUKO HAPO ULIPOGUSIA, SASA NIMEPATA PICHA. SUALA LA UTANZANIA DAMU HALINA MSINGI NI POINT YA KUITUPA KAPUNI. MTAJISUMBUA KUSEMA NINAMTETEA MISS TANZANIA KWANI NINAVYOONA HAPA HATUJIBU HOJA TUPO KUSHAMBULIA UHINDI NA YEYOTE ANAYEONYESHA KUWAKUBALI HAWA JAMAA KAMA RAIA WANAOSTAHILI KUSHIRIKIANA NASI JAPOKUWA NI WABAGUZI KWASABABU MLIZOTOA. BASI NAONA HATA IDI AMIN ALIFANYA SAWA KABISA KUWATIMUA UGANDA. INABIDI TUSHINIKIZE UONGOZI NA SERIKALI KUCHUKUA HATUA KWA HAWA JAMAA KWANI MPAKA WATOTO WAO WANAOZAA HAWAFAI NI WABAGUZI WANAJITENGA KAMA ILIVYOKUWA KWA MAKABURU AFRICA KUSINI. NAFIKIRI KAMA KUTOKUSHIRIKISHWA IWE KWENYE FANI ZOTE WALIZOJIINGIZA KAMA KUSUPORT MPIRA WA MIGUU N.K. MIMI FANI YANGU NI SOKA. NAFIKIRI WALE WAHINDI KAMA AKINA DEWJI NA MAREHEMU GULAMALI WASINGEFAA KUJIINGIZA KWENYE MCHEZO WETU KWANI NI WABAGUZI SANA SANA SANAAAAA!!!!!!HOJA YA HUYU MBAGUZI KUSHINDWA MISS UTALII HAINA MSINGI KWANI WATU HUJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA KUWEZA KUJISAHIHISHA NA KUFANYA VIZURI(MIFANO HAI IPO)

  36. Comment by Nana on October 7th, 2007 6:30 pm

    Asiyekubali kushindwa si mshindaji, Huko China hata fika kokote.

  37. Comment by Suleiman .M.-Majira on October 9th, 2007 1:53 am

    Serikali ‘yamfunda’ Richa Adhia

    Na Suleiman Mbuguni

    MISS Tanzania 2007, Richa Adhia ametakiwa kuwapuuza wanaombeza kutokana na ushindi wake na badala yake kuelekeza nguvu zake katika maandalizi ili afanye vizuri Miss World.

    Rai hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Dkt. Hermas Mwansoko ambaye alitembelewa na mnyange huyo ofisini kwake.

    Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Mwansoko alisema alishangazwa na baadhi ya watu waliopinga ushindi wa Richa baada ya kutangazwa kutwaa umalkia huo wa Tanzania.

    Mkurugenzi huyo alisema watu wanaombeza Richa ni wale ambao hawazijui kanuni za mashindano ya urembo ambazo zinatumetungwa na Serikali kupitia Baraza la Sanaa Taifa (BASATA).

    “Sisi tuliposikia eti Miss Tanzania hana nywele za kipilipili kwa kweli tulishangaa sana kwa kuwa mashindano haya hayana ubaguzi lakini hata hivyo licha ya kuzungumzwa mengi wao hawaelewi kanuni za mashindano ya ulimbwende.

    “Endapo kama wangezisoma kanuni zenyewe nina imani wasingepiga kelele lakini hata hivyo zisikubabaishe ichukulie kuwa changamoto kwako ya kufanya vizuri katika mashindano ya Dunia,” alisema Mkurugenzi huyo.

    Alimhakikishia mnyange huyo kuwa Serikali inamuunga mkono kwa silimia 100 ambapo alimtaka kutojiingiza katika machafu yatakayochafua jina lake.

    Mwansoko alimtaka Richa atakapokuwa nchini China kujichanganya na washiriki wenzake atakaowakuta huko ili na kuutangaza utamaduni wa Tanzania ili wauone Utanzania kupitia kwake.

    Naye Richa aliishukuru Serikali kwa kumuunga mkono katika kampeni zake za kushiriki mashindano ya Dunia, Miss World 2007 ambapo alisema atajitahidi kuhakikisha anafanya vema katika kinyang’anyiro hicho.

    mwisho.

  38. Comment by TanzanianDream on October 10th, 2007 2:38 am

    Hapa hata mmuunge miguu china hana jipya huyo atarudi na visingizio kuwa kabaguliwa…Heheh i wish abaguliwe tuone atakavyokuja kumtafuta mchawi wake na lundenga….

  39. Comment by JUMA20 on November 9th, 2007 3:23 am

    KWA NINI MISS TANZANIA HAKUNA UTARATIBU WA WANANCHI KUPIGA KURA KUMCHAGUA MSHIRIKI?! PENGINE INGELIONDOA MZOZO FULANI..

  40. Comment by abdullah on November 14th, 2007 1:47 pm

    Sasa unabenda shagua naani? Onuona biga klele mingi hivi tu? mhindi hii unosema yeye ni ya Tanzania
    Nani unobenda kuonewea bila haki,?
    Habana baguzi= washa hiyo maa’na sio mzuri
    Kama unashagua kwa haki iko maneno gani?

  41. Comment by danielle on December 4th, 2007 12:48 am

    jamani lundenga si ujiuzulu jamani,uwaachie wadau wengine mweh!!

  42. Comment by john mapinduzi on December 6th, 2007 12:21 am

    ninaoana imekuwa kawaida watu wakipewa dhamana kufanya dhamana kama ndio miliki,hivi huyu lundenga na makoye na kamati yao ni wakina nani hawa wasio na aibu hata kidogo,hivi ni mpaka lini watatoa visingizio visivyo na msingi?wajaribu kutoka waje watu wengine na “IDEALS” nyingine jamani mpaka tuwapige mtaani ndio mtajua mmetuchosha……….. ?ehhe

  43. Comment by jojo on December 7th, 2007 2:18 am

    Jamani swala la kutoshinda wala msi complain kwa sbabu kila kitu kiko wazi kwamba wenzetu wametuzidi tena sana si mliona wenyewewe jamani yaani wana nature ya urembo so sioni haja ya kumlaumu LUNDENGA na wala msitarajie hata cku moja eti tanzania yetu itakuja kutoa mrembo wa dunia ni ngumu labda vtaji vidogo2,ilo taji la Nancy bado ni muujiza kwetu

  44. Comment by carla on February 26th, 2009 5:49 am

    hey tsup every1 i wz saying tht wahindi ni watu wenye ubaguzi, wapo in our country lakin bado wajeuru, wanajifanya matajiri wakati if u go 2 india its one of poorest country in da world, i d’nt giv a damn abt them thus their ma friends

  45. Comment by trina on April 1st, 2009 7:54 am

    true carla n ts fyn 2 pips put their blames on idiot HL

Leave a Reply