
Hatutoshangaa hata kidogo ukituambia kwamba siku hizi unapowaongelea kina Michuzi ni vyema ukafafanua zaidi unamuongelea yupi. Kuna Ahmad na kuna Muhidin. Leo sisi tunamuongea Ahmad.
Ahmad Issa Michuzi (pichani) ambaye ni mhariri msaidizi wa jarida maarufu la burudani la KITANGOMA, mpiga picha hatari, ni mdogo wake Muhidin Issa Michuzi ambaye sifa zake sote tunazitambua.Huyu, tunaweza kusema, ni celebrity ambaye kivuli cha kaka yake wakati mwingine kinamziba. Lakini wakati huo huo kivuli hichohicho kina manufaa makubwa kwake, sio tu kuhusiana na ujuzi na ushauri bali pia na mengineyo mengi. Miezi kadhaa iliyopita aliamua kufuata vilivyo nyayo za kaka yake kwa kufungua blog yake ya picha ambayo imeshaanza kupata watembeleaji lukuki.
Katika kuthibitisha kwamba yeye ni gwiji na ameshakomaa sana tu katika fani ya upigaji picha, picha takribani zote zilizozagaa mtandaoni, zikiwemo zilizopo katika tovuti hii, kutoka katika msiba wa marehemu Mheshimiwa Amina Chifupa (R.I.P) yeye ndio mpigaji wake. Kama mhariri msaidizi wa KITANGOMA, mwajiriwa wa Prime Time Promotions, kijana ambaye kila siku kazi yake ni kuwasaka na kuzungumza na celebrities wa Tanzania, hususani wa fani ya muziki, ni lazima anakutana na mengi na pia anaona mengi. Nini maoni yake kuhusu sanaa hiyo ya muziki? Nini kimemsukuma kufungua blog yake? Je anajaribu kufuata nyayo za kaka yake au ana malengo tofauti? BongoCelebrity hivi karibuni ilifanya naye mahojiano yafuatayo;
BC: Jina Michuzi linafahamika hivi sasa kila kona ya dunia. Sababu inaeleweka. Kwa kifupi unaweza kutueleza Ahmad Michuzi ni nani?
A.MICHUZI: Ahmad Michuzi ni mjasiriamali, mpiga picha, blogger, mwanahabari, mcheshi, mchangamfu na mwelewa.Alizaliwa mjini TUKUYU mkoani Mbeya miaka 29 iliyopita.
BC: Umekuwepo kwenye uwanja wa entertainment kwa muda mrefu sasa. Unadhani mambo yanaendelea mbele au yanarudi nyuma? Sababu zozote?
A.MICHUZI: Ukweli ni kwamba mambo yanakwenda mbele zaidi kila kukicha kwa sasa, ukiangaalia kwa upande wa fani ya muziki, sasa hivi kumekuwepo na vijana wengi wengi na kila kukicha wanaongezeka kujikita kwenye fani hiyo, hali ambayo naamini imeleta changamoto kubwa hata kwa wanamuziki wakongwe.
Jambo lingine Wanamuziki wa sasa wanafaidika mno kuliko wanamuziki wa miaka ya nyuma, ukijaribu kufanya utafiti wa kawaida tu utabaini kwamba kimaendeleo wanamuziki wengi wa zamani walikuwa hawana maendeleo ya kutosha (wengine mpaka sasa), lakini hawa wa sasa wengi wao wameendelea kwa kujenga nyumba nzuri, kufunguo studio za kisasa na hata kuwa na magari ya kifahari.
Siwalaumu sana wanamuziki wa zamani nadhani hawakuweza kuwa na maendeleo ya kutosha inawezekana kutokana na mfumo uliokuwepo katika fani ya muziki kwa wakati huo.
Pia ukiangalia suala la mambo ya kurekodi muziki, upande wa hizi studio. Hapo zamani wanamuziki wa zamani walipata taabu sana katika suala zima la kurekodi nyimbo zao, lakini kwa sasa studio za kurekodia zimekuwa nyingi kila kona zikiwemo na za kisasa zaidi, nadhani hayo ni mafanikio makubwa sana.
Yote kwa yote lakini wanamuziki wa zamani wanabaki na heshima kubwa kupitia tungo zao zilizokuwa zimejaa dhana ya kuelimisha, kuburudisha na kuonya kwa namna ya kipekee, na nyimbo zao bado tamu na tunazisikiliza mpaka sasa tofauti na wanamuziki wa sasa ambao muziki wao mimi naufananisha na BIG G (kwamba unakubalika kwa muda mfupi sana baadae unapotea).
BC: Kama kijana wa kitanzania ni lazima ujishughulishe na mambo kadha wa kadha ili kieleweke. Hivi sasa unajishughulisha na nini zaidi?
A.MICHUZI: Kwa sasa najishughulisha na upigaji picha wa aina mbalimbali zikiwemo za sherehe ya aina yoyote ile, na pia ni mwandishi/ mhariri msaidizi na mpiga picha wa jarida la burudani la KITANGOMA na pia najihusisha na mambo ya graphics kwa kiasi fulani na ndio msimamizi mkuu wa usambazi wa jarida la KITANGOMA.
BC: Kama mhariri msaidizi wa gazeti la Kitangoma, unaweza kukumbuka ni story gani ambayo mmewahi kuichapisha na ambayo hutokaa uisahau daima?
A.MICHUZI: Kiukweli ni ya Marehemu Amina Chifupa, nakumbuka nilipata taabu kidogo kumpata (wakati huo) kutokana na yeye kuwa na harakati nyingi katika upande wa maisha yake.Nakumbuka nilimpigia simu tuonane kwa ajili ya kufanya mahojiano ya jarida letu, wakati huo Amina anawika kila kona ya jiji la Dar. Ilinichukua kama wiki huku nikimfuatilia, na hatimaye nikapata wasaa wa kuongea nae ana kwa ana , hakika niliongea nae mengi sana, hata ambayo kwa mlengo wa jarida langu haikuwa rahisi kuyaandika, hapo ndipo nilipomjua Amina alikuwa ni mtu wa aina gani.
Huwezi amini hilo jarida lilipotoka tu halikuchukua wiki likawa limekwisha kwa kununuliwa, na ndio kopi yetu iliovunja rekodi ya mauzo kuliko zote tulizowahi kuzichapisha mpaka leo.
BC: Kwa jinsi ambavyo jarida la Kitangoma linakuwa limesheheni habari motomoto kila linapotoka, wapenzi wasomaji wake wangependa kujua ni kwanini halitoki kila mwezi ili kujaribu kukidhi kiu ya wasomaji wake zaidi?
A.MICHUZI: Hata sisi tungependa sana liwe linatoka kila mwezi ili kukidhi haja ya wasomaji wetu. Kwa bahati mbaya kama wengi wenu mnavyofahamu ili kupata kitu kilicho bora maandalizi inabidi yawe mengi na ya muda mrefu. Tunawaomba sana radhi wasomaji wetu juu ya hilo.
BC: Nani msambazaji wa jarida la Kitangoma nje ya nchi kama Canada, Marekani, Uingereza na kwingineko?
A.MICHUZI: Hatuna msambazaji nje ya nchi mpaka dakika hii, lakini kama kuna mtu/kampuni yeyote akijitokeza tunaweza kuweka mambo mezani na tukafanya kazi, hivyo wanakaribishwa sana
BC: Pamoja na kuwa mhariri msaidizi wa gazeti la Kitangoma, wewe pia ni mfanyakazi wa Prime Time Promotions.Unaweza kutuambia unafanya kazi gani pale?
A.MICHUZI: Kikubwa ni usimamizi, maandalizi na uangalizi wa jarida la KITANGOMA katika kuhakikisha linatoka kwa muda uliopangwa,liko katika kiwango kinachotakiwa na mambo kama hayo.
BC: Ni changamoto gani mnazokumbana nazo mara kwa mara katika chumba cha uhariri cha jarida la Kitangoma?
A.MICHUZI: Changamoto kubwa ni ucheleweshwaji wa kutopata matangazo kwa muda muafaka, mengineyo ni ya kawaida tu.
BC: Kwa sababu jarida la Kitangoma limejikita zaidi katika kuandika masuala ya muziki na wanamuziki, kwa vyovyote vile kila kukicha unakutana na wasanii wa aina mbalimbali za muziki na kama sikosei zaidi wasanii wa muziki wa kizazi kipya au Bongo Flava. Nini maoni yako kuhusiana na muziki huu? Unaweza siku moja kuwa kitambulisho chetu rasmi nje ya nchi?
A.MICHUZI: Kama nilivyosema hapo awali, muziki wa sasa unalipa ! ila kikubwa na cha muhimu sana ni kuishauri serikali itupie macho na ipeleke nguvu za kutosha katika suala zima la kupambana na wizi wa kazi za wasanii, suala hili limekuwa sugu mno japokuwa kuna chombo husika cha hakimiliki (COSOTA),lakini bado tunakutana na wasanii wengi wengi ambao ukifanya nao mahojiano bado wananahoji uwepo wa chombo hicho ni nini ?
Suala lingine ni kuhusu Wasambazi wa kazi za wasanii, kama kuna wadau wenye uwezo wa kusimamia ama kufanya kazi ya usambazaji wa kazi za wasanii kwa wakati huu wanatakiwa wajitokeze,kwani kumekuwepo na lawama lukuki kuhusiana na suala usambazaji wa kazi za wasanii kwa ujumla.
Nakumbuka nilikuwa nafanya mahojiano na prodyuza wa studio fulani ya hapa jijini Dar, nae kilio chake kikubwa alichonieleza ni suala la wasambazaji kulipa ujira mdogo sana kwa wasanii wakati asilimia kubwa ya kazi wanaifanya wao, akanitolea mfano Msambazaji anatoa kanda na kuiuza kati ya sh 1200 mpaka 1500 lakini msanii anapata 200 tu, akiuza CD kati ya sh 7000 hadi 10,000 msanii anapewa kiasi cha sh 500, je kwa mtazamo tu wa kawaida ni HAKI ? Je uwiano wa kazi hapo uko wapi wadau ??? !!!
TUBADILIKE BWANA ILI KILA MMOJA AFAIDI MATUNDA YA JASHO LAKE. Hapo ndipo tutawawezesha wasanii kuwa wabunifu zaidi na kisha kutupa kitambulisho nje ya nchi kwa upande wa muziki.
BC: Nini uhusiano wa jarida la Kitangoma na kampuni ya Prime Time Promotions?
A.MICHUZI: Prime Time Promotions ndio inayomiliki jarida la Kitangoma.
BC: Hivi karibuni umeanzisha blog ya picha ambayo imeshaanza kupata watembeleaji wengi tu. Nini kimechangia katika uamuzi wako wa kuanzisha blog?
A.MICHUZI: Kwanza Michuzi ambaye mara nyingi mimi hupenda kumuita MKUU, ndiye aliyenifanya nianzishe hii blog yangu ya picha. Kimsingi namshukuru sana sana kwa kunihamasisha katika hili. Pili ni mimi mwenyewe kuwa na hazina kubwa ya matukio ya picha ambayo hata wakati mwingine inatokea hakuna mpiga picha mwingine mwenye picha hizo zaidi ya mimi.Kwa hiyo baada ya kuhamasishwa na MKUU nikaona kwa nini nisifanye hivyo na mimi nikaanza kuielimisha jamii kwa njia ya picha.
BC: Kwanini umeamua kuuita blog yako JIACHIE?
A.MICHUZI: Nimeamua kuiita hivyo kutokana na mandhari ya picha zangu nyingi ni za namna hiyo,pia hata kwenye suala la watoa maoni nahisi nimewapa hamasa zaidi ya kujiachia kwa lolote lile,watu wanatakiwa waziachie hisia zao, mawazo yao kuhusiana na picha husika, kikubwa ni kuepuka lugha isiyofaa. Hilo ndio la jambo la msingi zaidi.
BC: Unadhani blog zinaweza kuwa na mchango gani katika kuleta mabadiliko ya kijamii ambayo nchi kama Tanzania inayahitaji sana?
A.MICHUZI: Blog zinaweza kuleta mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko hapa nchini, mfano blog ya MKUU (Michuzi) na nyinginezo naamini kwa njia moja ama nyingine zimeleta mabadiliko mengi tu kwa baadhi ya watu (ingawa hatuwezi kuwajua kwa idadi, lakini hilo lipo), kuna baadhi ya mambo yakiwemo ya kisiasa na kijamii yamewekwa wazi ili kuisaidia jamii husika iamue katika suala la maamuzi yake kutokanana sula husika.Yapo mengi lakini hayo ni kwa uchache tu.
BC: Upigaji picha ni kitu ambacho hivi sasa tunaweza kusema kimo kwenye damu ya akina “Michuzi”. Ulianza lini utundu huu wa kupiga picha? Unaikumbuka picha yako ya kwanza kupiga?
A.MICHUZI: Daaa nakumbuka nilianza utundu wa kupiga picha toka nasoma sekondari nikiwa kidato cha pili, nakumbuka ilikuwa mwaka 1995 nikiwa na camera ndogo aina ya yashica.Sio siri wanafunzi wenzangu walikuwa wakiniamini katika upigaji picha lakini sikujua ni kwa nini, wakati huo mimi najua kuwasha camera na kupiga tu lakini sikujua kama kuna zaidi ya hapo.
Nakumbuka picha yangu ya kwanza kuipiga ambayo pia iliwahi kutumika kwenye gazeti la serikali la UHURU ,ilikuwa ni ya wale askari kanzu wakiwa wamewakamata machinga viwanja vya mnazi mmoja huku vurugu nyingi zikiwa zimetawala.
BC: Katika nchi za magharibi, makampuni mengi makubwa yakiwemo yale ya habari kama CNN, BBC, FOXNEWS,ABC, NBC nk sio tu yanaheshimu mchango wa blogs, bali pia yameanzisha huduma mbalimbali za blogs. Kwa maoni yako,makampuni ya Tanzania yanaweza kujifunza nini kutokana na muelekeo huo?
A.MICHUZI: Ni jambo la kimaendeleo zaidi hivyo hata makampuni yenyewe ya hapa Tanzania yanapaswa kubadilika kwa kuiga na kujifunza kutoka kwa wenzao kama ulivyosema hapo juu, yanapaswa kuanzisha blogs zao ili kuongeza ama kuleta changamoto katika suala zima la kupashana habari kila kona ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
BC: Jarida la Kitangoma lina mpango wowote wa kuanzisha blog yake ili wasomaji wawe na nafasi zaidi ya kuchangia na kutoa maoni yao?
A.MICHUZI: Ndio hapo awali tulianzisha blog, ila tunasikitika kulitokea matatizo ambayo kidogo yalituletea mabadiliko,lakini bado tuna mpango huo tena wa kuendelea nayo.
BC: Nini mipango yako binafsi katika miaka kumi ijayo?
A.MICHUZI: Mipango yangu binafsi nataka kujiendeleza zaidi na mambo ya upigaji picha (photography) na Graphics kwa upana zaidi.
BC: Kuna lolote ambalo ungependa kuliongelea ambalo hatujakuuliza?
A.MICHUZI: Sina la zaidi ya kuwashukuru ninyi na wanablog wenzangu kwa kuanza kuniunga mkono katika ulimwengu huu wa blog. wachanga tuko wengi lakini naomba tupeane moyo ikiwezekana hata kusaidiwa kimawazo ama kwa vyovyote vile ili tuweze kutimiza ndoto zetu za pale tunapotaka kufika na kuijenga nchi yetu ya Tanzania.
BC: Shukrani Michuzi Jr na tunakutakia kila la kheri katika yote.Asante,!
Kwa picha za matukio mbalimbali tembelea blog yake michuzijr.blogspot.com.
Feedback / Comments
11 Responses to “WATU WAZIACHIE HISIA ZAO-MICHUZI JR”
Leave a Reply


Big up Michuzi Jr.Nimeitembelea blog yako na pia ni mpenzi wa jarida lenu la Kitangoma…mwaaaaa
Michuzijr…
kama nilivyopokea waraka wakooo mkuu…
kazi ni mojaaa tuu kuliendelezaa..
nakupa big Up kwa Ushukiano wako mkubwaa..
Usijali ”Kitaeleweka TU..!!
Admin
http://www.haki-hakingowi.blogspot.com
Mie naomba kumuuliza huyu Mpakanjia alichokua anahuzunika ni nini na ikiwa tunasikia alishaoa hata kabla Amina hajafa, jamani wanaume muache kusikiliza maneno na muyafanyie uchunguzi maneno kabla ya kuamua, roho hainunuliwi lakini ingekua inanunuliwa tungeinunua roho ya Amina kwa bei yeyote ile.
Huyu nae ni celebrity? kuwa seriuos mzee tutaanza kukimbia hapa.
Follow nyayo za bro wako Muhidini. Kazi unazofanya zinaridhisha.
fin man,tumekuona sasa tupe mi-nuz tunakusubiri kwa hamu.shwanga!
hiki ni kioo cha muhidini..jr kaza buti kaka kitaeleweka tu,na kuhusu mswala ya wasanii na haki zao hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu sana kwa wasanii wa TnzniA..KWA KWELI Muziki wetu unalipa na hata serikali inajua hayo ila tatizo ni pale when comes time for who has to stand for us..artist.. viongozi wana gwaya gwaya.. kwani hawajui huu muziki unaweza hata kusaidia nchi katika sekta za uchumi.kama vile marekani.. 45%ya uchumi wa marekani unatokana na entertaiment..kama vile film industries,music companies,.nk so tz tunatakiwa kuiga mifano ya nchi fulani vilevile tunapaswa kuvisamini vya nyumbani…mdau …xl.. d masterd. nl
hi michuzi nafurahi sana kwa kuanzisha web hii inanifanya niweze kupata ujumbe mbalimbali wa kupata data ulimwenguni cha msingi endelea kuiboresha sana thanks
hivi michuzi junior umesoma wapi hakyamungu hii sura kama naijua hivi ila sikumbuki wapi sijui chuo sijui shule sijui wapi kaka angu
BIG UP MICHUZIS FAMILY INAONESHA KIASI GANI MLIVYO ACTIVE KWENYE MABO YA HABARI.INAPENDEZA SANA TU HII NI FANI YENU MSIITUPE ENDELEENI KUTUPA HABARI MOTOMOTO.
poa jitahid